02. Aina tatu za subira


Wanachuoni wanasema kuwa subira imegawanyika aina tatu:

1- Kuwa na subira juu ya kumtii Allaah.

2- Kuwa na subira juu makatazo ya Allaah.

3- Kuwa na subira juu ya makadirio ya Allaah yenye kuumiza.

Aina ya kwanza ni subira juu ya kumtii Allaah. Ni kule mtu kutekeleza yale aliyoamrishwa na Allaah (Ta´ala) japokuwa ni mazito kwake. Hata kama nafsi yake inataka kustarehe anatakiwa kusubiri. Matokeo yake anadhibiti vipindi  vitano vya swalah, anaamka na kwenda kuswali Fajr, anaamka na kusimama kuswali swalah ya usiku na anafunga na kuacha chakula, kinywaji na jimaa – yote haya kwa ajili ya kumtii Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Anapambana katika njia ya Allaah na kusubiri juu ya majeraha na maumivu yanayosababishwa na maadui. Anatakiwa kuwa na subira juu ya kumtii Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala), kwa sababu ndani ya utiifu ni lazima kuchoka.

Aina ya pili ni subira juu ya makatazo ya Allaah. Mtu anatakiwa kujiepusha na yale Allaah (Ta´ala) aliyomkataza. Wakati nafsi inamvuta na kutaka shahawa zilizoharamishwa yeye anafanya subira kwa kuizuia. Japokuwa mashaytwaan wa kibinadamu na wa kijini wanampambia vitu vibaya, lakini yeye anaizuia mbali nafsi yake na yale aliyoharamisha Allaah.

Aina ya tatu ni subira juu ya makadirio ya Allaah yenye kuumiza. Mtu akishikwa na maradhi au akapatwa na msiba juu ya mali yake au mtoto wake au ndugu yake, anasubiri na wala hakati tamaa. Kufanya hivi ni katika imani. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَبَشِّرِ الصَّابِرِينَ الَّذِينَ إِذَا أَصَابَتْهُم مُّصِيبَةٌ قَالُوا إِنَّا لِلَّـهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ

“Wabashirie wenye kusubiri ambao unapowafika msiba basi husema: “Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake ni wenye kurejea.”[1]

Wanatambua kuwa msiba umetoka kwa Allaah na kwamba ni kutokana na mipango na makadirio ya Allaah na kwa ajili hiyo hawakasiriki na wala hawavunjiki moyo.

Kuhusiana na makadirio ya Allaah yasiyokuwa yenye kuumiza yanayopendwa na nafsi, hayahitajii subira, kwa sababu nafsi ni yenye kumiliki juu yake.

[1] 02:155-156

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: I´aanat-ul-Mustafiyd bi Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 430-431
  • Imechapishwa: 13/08/2019