Himdi zote zinamstahikia Allaah, Mola wa walimwengu. Swalah na salaam zimwendee Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake wote.

Amma ba´d:

Hakika Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameeleza kuwa kutatokea mgawanyiko katika Ummah huu kama ilivyotokea katika nyumati zilizotangulia. Pindi yatatokea hayo akatuusia kushikamana na yale aliyokuwa akifuata yeye (Swalla Allaahu ´alyhi wa sallam) na Maswahaba wake (Radhiya Allaahu ´anhum). Amesema (Swalla Allaahu ´alyhi wa sallam):

“Mayahudi wamegawanyika katika mapote sabini na moja, manaswara wakagawanyika katika mapote sabini na mbili na Ummah wangu utagawanyika mapote sabini na tatu. Yote hayo yataingia motoni isipokuwa moja tu.” Kukaulizwa: “Ni kina nani, ee Mtume wa Allaah?” Akasema: “Ni lile litakalofuata yale ninayofuata mimi hii leo na Maswahabah zangu.”

“Hakika yule atakayeishi katika nyinyi basi atakuja kuona tofauti nyingi, basi jilazimieni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu waongofu baada yangu. Shikamaneni nazo barabara na yaumeni kwa magego. Tahadharini na mambo ya kuzua! Hakika kila kitachozushwa ni Bid´ah na kila Bid´ah ni upotevu.”

Katika upokezi mwingine imekuja:

“… na kila upotevu ni Motoni.”

Namna hii ndivyo katuusia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kushikamana na yale aliyokuwa akifuata yeye na Maswahabah wake wakati pindi kutatokea migawanyiko.

  • Mfasiri: Firqatunnajia.com