´Allaamah na hoja ya Uislamu Abu Ja´far al-Warraaq at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema Misri:

1- Huu ni ubainifu wa ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah kwa mujibu wa madhehebu ya wanachuoni wa Uislamu Abu Haniyfah an-Nu´maan bin Thaabit al-Kuufiy, Abu Yuusuf bin Ibraahiym al-Answaariy na Abu ´Abdillaah Muhammad bin al-Hasan ash-Shaybaaniy na yale wanayoamini katika misingi ya dini na kumuabudu kwayo Mola wa walimwengu – Allaah awawie radhi.

MAELEZO

Hakika ´Aqiydah ndio msingi wa dini na ambayo imekusanya kuhushudia ya kwamba hapana mwabudi wa wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah. Shahaadah ndio nguzo ya kwanza ya Uislamu. Ni wajibu kuitilia umuhimu, kuijali na kuitambua. Vilevile ni wajibu kutambua vile vinavyoitia kasoro ili mtu awe juu ya yakini na juu ya ´Aqiydah sahihi. Kwa sababu muda wa kuwa dini imejengwa juu ya ´Aqiydah sahihi, basi inakuwa ni dini iliyonyooka na yenye kukubaliwa mbele ya Allaah. Ikisimama juu ya ´Aqiydah yenye kutikisika, yenye kuyumbayumba na ilioharibika basi dini inakuwa si sahihi na isiyokuwa na msingi. Kwa ajili hiyo ndio maana wanachuoni (Rahimahumu Allaah) wametilia umuhimu suala la ´Aqiydah na hawakuchoshwa kuibainisha katika darsa na vitabu. Hivyo ndivyo ilivyopokelewa karne na karne.

Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) hawakuwa na mashaka yoyote juu ya yale yaliyomo katika Qur-aan na Sunnah. ´Aqiydah yao ilikuwa yenye kujengeka juu ya Qur-aan na Sunnah. Hawakuwa na shaka wala kusimama. Walikuwa ni wenye kuamini na kuyachukulia dini yale yaliyosemwa na Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hawakuwa ni wenye kuhitajia utunzi wa vitabu, kwa sababu ´Aqiydah yao ilikuwa ni jambo wanajisalimisha kwalo na la kukata – ´Aqiydah yao ilikuwa ni Qur-aan na Sunnah. Mfumo huohuo ukafuatwa na wanafunzi wao, Taabi´uun, ambao walijifunza kutoka kwao. Kwa hiyo hakukuwa na mizozo yoyote katika ´Aqiydah. Kila kitu kilikuwa katika nidhamu na marejeo yao ilikuwa Qur-aan na Sunnah.

Wakati kulipozuka mapote na tofauti, watu walio na ´Aqiydah mbovu, fikira zilizopinda au ambao ´Aqiydah yao haijakita kwenye moyo, fikira zilizopinda, walipoingia katika Uislamu, watu wakawa wanarudi katika misingi na mifumo ya wapotevu badala ya Qur-aan na Sunnah, hapo ndipo maimamu wakalazimika kubainisha ´Aqiydah sahihi, kuiandika, kuitunga na kuipokea kutoka kwa maimamu wa Ummah. Kwa hiyo wakaandika vitabu vya ´Aqiydah ambavyo vikawa ni marejeo kwa wale waliokuja baadaye mpaka kitaposimama Qiyaamah. Hivi ndivo Allaah (Ta´ala) alivoihifadhi na kuilinda dini hii. Amefanya watu waaminifu wanaifikisha kama ilivyotajwa katika Qur-aan na Sunnah na kuraddi upotoshaji wa watu wa batili na ushabihisho wa wengine. Hivo ndivo ikawa inarithiwa ´Aqiydah hii karne baada ya karne.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 23-25
  • Imechapishwa: 05/08/2018