01. Utangulizi wa ”Bayaan-ul-Ma´aaniy”


Huu ni utangulizi wa Imaam na Haafidhw ´Abdullaah bin ´Abdir-Rahmaan bin Abiy Zayd al-Qayrawaaniy ambao aliandika juu ya kitabu chake katika madhehebu ya Maalik. Hapo kitambo Salaf (Rahimahumu Allaah) walikuwa na mazowea pindi wanapotunga tungo za Fiqh basi huanza na ´Aqiydah. Walikuwa wakiigawanya Fiqh mafungu mawili; Fiqh kubwa katika ´Aqiydah na Fiqh katika mambo ya matawi nayo ni ile Fiqh katika mambo ya ´ibaadah na mambo ya miamala. Kwa sababu Uislamu unazo nguzo tano: Kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa kweli isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, kusimamisha swalah, kutoa zakaah, kutoa zakaah, kufunga Ramadhaan na kuhiji nyumba ya Allaah tukufu.

Nguzo ya kwanza katika nguzo za Uislamu ni ´Aqiydah; kuamini nguzo sita za imani. Kumuamini Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Yake, siku ya Mwisho na Qadar kheri pamoja na shari yake. Kwa ajili ya kubainisha nguzo hii walikuwa wakitunga vitabu vya ´Aqiydah sahihi kwa mujibu wa madhehebu ya Salaf. Kisha baada ya hapo wanatunga kufafanua nguzo nne: swalah, zakaah, funga na hajj na yanayofuatia hayo katika miamala, wasia, waqfu, mirathi, jinai na hukumu. Lakini zama zilivyokuwa zinaenda wakaipambanua Tawhiyd kivyake na ´ibaadah na yale yote yanayohusiana nayo kivyake. Kama hali ilivyo hii leo juu ya vitabu vilivyotungwa juu ya madhehebu manne.

Miongoni mwa tungo hizo ni kitabu ”ar-Risaalah” cha Ibn Abiy Zayd. Amekitunga juu ya Fiqh ya Imaam Maalik. Kama walivyofanya wanachuoni wa mwanzo amekianza na Tawhiyd. Wanachuoni wametilia umuhimu kitabu hiki hali ya kukifafanua, kukiweka wazi, kukihifadhi na mpangilio. Kwa sababu ni kifupi, muhimu na kimesalimika kutokamana na makosa. Isitoshe kimeandikwa kwa mujibu wa madhehebu ya Salaf. Pia kimefafanuliwa kwa njia ya upindaji na kukipindisha ili kiendane na madhehebu ya waliokuja nyuma, lakini maelezo yake ya kale na yaliyokuja baadaye hali ya kufuata nyayo zao yamesalimika.

Wale maimamu wanne, na kadhalika waliokuwa kabla yao, walikuwa juu ya mfumo wa Salaf. Vilevile wanafunzi wao ambao wamejifunza kutoka kwao walikuwa juu ya madhehebu ya Salaf inapokuja katika ´Aqiydah, ´ibaadah na mambo mengine ya dini. Hali iliendelea hivo hadi ilipofika mwishoni mwa karne ya nne. Kuanzia hapo ndipo kulianza kuingia ya kuingia kwa waislamu. Kulizuka Suufiyyah. Kulizuka waabudia makaburi. Kulizuka wanafalsafa na watu wa mantiki. Watu waliathirika na Suufiyyah, waabudia makaburi, madhehebu ya Shiy´ah na falsafa. Wakaacha kujengea hoja kwa Qur-aan na Sunnah na wakajengea hoja kwa falsafa, mantiki na mjadala. Wakaita kuwa ni hoja za kiakili. Kuhusu dalili za Qur-aan na Sunnah wakaziita kuwa ni dalili za kudhania. Wao wanaona kuwa zinatia dhana ilihali mantiki na falsafa zinafidisha yakini na ndio maana wakaita kuwa ni hoja za kiakili. Hivyo wakaitanguliza akili juu ya andiko la kiwahyi. Hoja yao wanasema kuwa akili haikosei tofauti na andiko la kiwahyi ambalo linaweza kusibiwa na unyonge wa cheni za wapokezi, unyonge wa wapokezi na mengineyo. Wanaeneza mashaka juu yake na wakazijenga ´Aqiydah zao juu ya mambo haya.

Baadhi ya wafuasi wa madhehebu manne wamesibiwa na jambo hili. Kwa mfano utampata mtu anayesema kuwa yeye anafuata madhehebu ya Shaafi´iy katika Fiqh lakini inapokuja katika ´Aqiydah anamfuata mtu mwingine. Anaweza kusema kuwa yeye anafuata madhehebu ya Shaafi´iy na wakati huohuo yeye ni Naqshbandiy katika ´Aqiydah. Yeye anamfuata Shaafi´iy katika Fiqh lakini inapokuja katika ´Aqiydah yeye ni Naqshbandiy. Jambo hili limekuwa la kawaida kwao mpaka wakafikia kupinda kutoka katika ´Aqiydah za maimamu wao na wakachukua ´Aqiydah za vile vizazi vilivyokuja nyuma. Wamekuwa hawako wazi kama khunthaa; hawatambuliki kama ni wanamme au wanawake? Huu ni ugonjwa uliowapata waislamu. Kutokana na sababu hiyo wakajenga majengo juu ya makaburi na nyoyo zikafungamana nayo na wakaihama misikiti.

Wakati Faatwimiyyah (ambao ni Shiy´ah Baatwiniyyah) waliposhika utawala Misri na misikiti mingine na zikaenea twuruq za Suufiyyah, ndipo wakaanza kujenga makuba juu ya makaburi na kuyainua. ´Aqiydah za watu wengi zikabadilika. Kwa kiasi kikubwa Uislamu ukabaki ni jina pasi na uhakika. Licha ya hayo Allaah huwatoa maimamu katika wahuishaji. Wanalingania katika mfumo wa Salaf na kubainisha yale mapungufu na ukiukaji unaopatikana katika madhehebu ya wenye kwenda kinyume. Miongoni mwao ni Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah, Ibn-ul-Qayyim na Salafiyyuun wengi ambao ni Muhaddithuun. Watu hawa ni wahuishaji. Kwa sababu Allaah kila baada ya miaka mia hutuma juu ya Ummah huu mtu ambaye atahuisha dini yao[1]. Himdi zote ni stahiki ya Allaah ambaye daima hufanya kuwepo kwa ambaye anainusuru dini hii, akalingania kwayo na kuibainisha kwa watu. Hata kama giza limetawala sehemu kubwa na madhehebu yaliyopinda yamekita kwa waislamu, Allaah (´Azza wa Jall) huinusuru dini Yake na hufanya daima kuwepo ambaye anaihuisha, akalingania kwayo na kuwabainishia nayo watu. Hii ni fadhilah na wema kutoka kwa Allaah. Lakini upindaji umetawala sehemu kubwa ya ulimwengu wa Kiislamu. Miongoni mwa hayo ni upindaji katika ´Aqiydah. Wameacha ´Aqiydah ya Salaf na wakashika ´Aqiydah ya wale waliokuja nyuma iliyojengeka juu ya mantiki na falsafa. Wamejenga ´Aqiydah na vitabu vyao juu ya mambo haya. Wanayasoma na kuyafunza katika misikiti, masomo na vyuo vyao.

Utangulizi wa Ibn Abiy Zayd ni katika mapambano ya mwanzomwanzo makubwa yaliyojengeka juu ya madhehebu ya Salaf. Mtunzi alikuwa akiishi katika zile karne za mwanzo, ni katika watu wa karne ya nne. Alikuwa akifuata ´Aqiydah ya Salaf aliyoisoma kwa waalimu zake. Alikuwa ni bingwa katika madhehebu ya Imaam Maalik na marejeo kwayo. Mpaka akapewa jina ”Maalik mdogo” kwa sababu ya umairi wake katika madhehebu na ´Aqiydah. Aidha watu walikuwa wakimwamini. Miongoni mwa tungo zake ni kitabu hiki na utangulizi wake.

Ni utangulizi wenye thamani mno. Sababu ya kukitunga na tungo nyenginezo ni kwamba mmoja katika waalimu zake wa Qur-aan alimwomba atunge kitabu juu ya Fiqh ya madhehebu ya Imaam Maalik ili kiwe mikononi mwa wanafunzi wakisoma na wakihifadhi. Akaitikia maombi ya mwalimu wake ambapo akatunga kitabu hiki na utangulizi wake. Kitabu hiki na utangulizi wake vikaanguka mikononi mwa wanafunzi na wakafurahi kwavyo. Vikaenea na wanafunzi wakawa wanafunzwa navyo katika masomo ya Qur-aan na mengineyo. Haya ni kutokana na baraka za uhakiki na nia njema. Mazingatio sio ukubwa wa kitabu na mijeledi mingi. Kinachozingatiwa ni kwamba kitabu kimebeba elimu sahihi na utakasifu wa nia ya mtunzi kwa Allaah (´Azza wa Jall), ijapo kimeandikwa kwa ufupi. Kitabu hiki kina karatasi chache. Hata hivyo kimepata umaarufu mkubwa kutokana na ule uhakiki, elimu sahihi na nia njema ya mtunzi na kumtakasia kwake nia na nasaha yake kwa ajili ya Allaah (´Azza wa Jall). Namna hii ndivo Allaah humtunuku mwanachuoni muhakiki kwa kuweka baraka katika elimu yake na katika tungo zake ijapo zitakuwa ndogo na chache.

[1] Abu Daawuud (4293).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 7-10
  • Imechapishwa: 29/06/2021