01. Utangulizi wa “al-Qadhwaa´ wal-Qadar”

Himdi zote anastahiki Allaah. Tunamhimidi Yeye na kumuomba msaada na msamaha. Tunaomba ulinzi kwa Allaah kutokamana na shari ya nafsi zetu na matendo yetu maovu. Yule anayeongozwa na Allaah, basi hakuna wa kumpoteza, na yule anayepotezwa na Allaah, basi hakuna wa kumwongoza. Ninashuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah, hali ya kuwa peke yake hana mshirika, na ninashuhudia ya kwamba Muhammad ni mja na ni Mtume Wake. Allaah (Ta´ala) amemtuma kabla ya Qiyaamah ili kufikisha bishara njema na kutahadharisha na akiwa ni mlinganizi katika dini ya Allaah na taa lenye kuangaza. Akafikisha ujumbe, akatimizia amana, akaunasihi Ummah na akapambana kwa ajili ya Allaah ukweli wa kupambana mpaka pale alipofariki. Swalah na salaam ziwe juu yake yeye, kizazi chake, Maswahabah wake na wale wote watakaomfuata mpaka siku ya Qiyaamah.

Amma ba´d:

Ndugu watukufu! Hakika katika mkutano huu tutaitafiti mada muhimu inayowahusu waislamu wote. Inahusiana na makadirio na mipango ya Allaah. Jambo hili liko wazi. Tusingelizungumzia endapo watu wengi wasingeuliza maswali juu yake, lau yasingekuwa ni yenye kuwatatiza watu wengi, lau kama wengi wasingelikuwa ni wenye kuyaingilia (wakati fulani kwa haki na wakati mwingine kwa batili), lau kama matamanio yasingelikuwa ni yenye kuenea na ni mengi na lau kama mtenda dhambi asingelikuwa ni mwenye kutaka kuyapitisha madhambi yake kwa kutumia hoja ya makadirio na mipango.

Kipindi chote hakukuacha kuwa maoni tofauti kuhusu makadirio na mipango. Imepokelewa namna ambavyo Maswahabah walizozana kuhusu makadirio ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawakataza na kuwaambia kwamba hakuna kilichofanya kuangamia nyumati zilizotangulia isipokuwa ni sampuli ya mizozo kama hii. Hata hivyo Allaah amewaongoza waja wake waumini Salaf ambao wamechukua njia ya kati na kati katika elimu na maneno yao.

Makadirio na mipango ya Allaah (Ta´ala) ni katika uola Wake (Subhaanahu wa Ta´ala) juu ya waja Wake. Ni moja katika vigawanyo vya Tawhiyd ambavyo wanachuoni wamevigawanya mafungu matatu:

1- Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah inayohusiana na kumpwekesha Allaah katika ´ibaadah.

2- Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah inayohusiana na kwamba Allaah peke yake ndiye mwenye kuumba, mwenye kumiliki na mwenye kuyaendesha mambo.

3- Tawhiyd-ul-Asmaa´ was-Swifaat inayohusiana na kwamba Allaah amepwekeka katika majina na sifa Zake.

Kuamini makadirio ni katika uola wa Allaah (´Azza wa Jall), Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah. Ndio maana Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amesema:

“Makadirio ni uwezo wa Allaah.”

Kwa kuwa bila shaka yoyote ni katika uwezo Wake wenye kuenea. Makadirio vilevile ni siri ya Allaah (Ta´ala) iliyofichikana ambayo hakuna yeyote anayeijua isipokuwa tu Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala). Yameandikwa katika ubao Uliohifadhiwa ambao hakuna yeyote aliye nao. Hatujui yale Allaah aliyotukadiria juu yetu au dhidi yetu. Vilevile hatujui yale Allaah aliyowakadiria viumbe isipokuwa baada ya kile kilichokadiriwa kutokea au kupitia maelezo sahihi.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Qadhwaa’ wal-Qadar, katika Majmuu´-ul-Fataawaa (5/215-216)
  • Imechapishwa: 25/10/2016