01. Ulazima wa kuyaheshimu makaburi ya waislamu na kutoyatweza

Himdi zote njema anastahiki Allaah Mmoja pekee. Swalah na amani zimwendee yule ambaye hakuna Nabii mwingine baada yake; Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake.

Amma ba´d:

Nimepokea jumbe nyingi ambazo maudhui yake ni pamoja na kukemea yale yanayofanywa na baadhi ya watu ambapo wanayatweza makaburi na kutoyaheshimu. Ndipo nikaona niandike juu ya hayo maneno haya mafupi kwa ajili ya kuzindua na kutahadharisha. Lengo ni kwa ajili ya kunasihi kwa ajili ya Allaah na waja Wake. Nasema:

Zipo Hadiyth nyingi Swahiyh kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya ulazima wa kuwaheshimu waislamu waliokufa na kutowaudhi. Hapana shaka yoyote kwamba kupitisha juu yao magari, matrekta, mifugo na kutupa taka juu yao yote hayo ni kuyatweza na kutowaheshimu. Aidha yote hayo ni kumuasi Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na pia ni kuwadhulumu waliokufa na kuwafanyia uadui. Kumethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) makatazo na kutahadharisha yaliyo chini ya hayo kama vile kukaa juu ya kaburi, kuliegemea na mfano wake. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Msiswali kuyaelekea makaburi na wala msiketi juu yake.”[1]

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema tena:

“Mmoja wenu kukaa juu ya kaa ambapo likachoma nguo yake na kuiondoa ngozi yake ni bora kwake kuliko kukaa juu ya kaburi.”[2]

Ameipokea Muslim tena.

´Amr bin Hamz amesimulia:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliniona nimeliegemea kaburi ambapo akasema: “Usimuudhi mtu mwenye kaburi hili.”[3]

Ameipokea Imaam Ahmad.

Ni lazima kwa waislamu wote kuyaheshimu makaburi ya wafu wao na kutoyaweka kwa chochote katika madhara, kama vile kukaa, kupitisha gari na kutupa taka juu yayo na mfano wa madhara mengine kama hayo.

[1] Muslim (972).

[2] Muslim (971).

[3] Ahmad (2795).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tahdhiyr min Fitnat-il-Qubuur, uk. 3-4
  • Imechapishwa: 06/04/2022