Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Kwa jina la Allaah, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu

Ninamuomba Allaah Mkarimu, Mola wa ´Arshi tukufu, akuhifadhi duniani na Aakhirah na akufanye ni mbarikiwa popote utapokuwa. Vilevile akufanye kuwa ni miongoni mwa wale wanapopewa basi hushukuru, wanapopewa mtihani basi husubiri na wanapotenda dhambi huomba msamaha. Hakika mambo haya matatu ndio ufunguo wa furaha.

MAELEZO

Hii ni “al-Qawaa´id al-Arbaa´ah” [misingi minne] iliyoandikwa na Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah).

Ni kitabu cha kipekee ambacho huwa kinachapishwa pamoja na “Thalaathat-ul-Usuwl” kwa sababu ya kuhitaji kwavyo na ili viwe mikononi mwa wanafunzi.

“Qawaa´id” ni wingi wa neno “Qaa´idah”, likiwa na maana ya msingi ambao kwao hutoa mambo na matawi mengi.”

Kanuni hizi nne zilizotajwa na Shaykh (Rahimahu Allaah) ndani yake mna utambuzi kuhusu Tawhiyd na shirki.

Ni ipi kanuni katika Tawhiyd? Ni ipi kanuni katika shirki? Kwa sababu watu wengi wanachanganya mambo haya mawili. Wanachanganya maana ya Tawhiyd na kuuliza ni kitu gani. Vivyo hivyo wanachanganya maana ya shirki na kuuliza ni kitu gani. Kila mmoja anafasiri mambo haya mawili kwa mujibu wa matamanio yake.

Lililo la wajibu kwetu ni kuirudisha misingi yetu katika Qur-aan na Sunnah, ili msingi huu uwe salama, sahihi na uwe umechukuliwa kutoka katika Kitabu cha Allaah na Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hili khaswa katika mambo haya mawili makubwa; Tawhiyd na shirki.

Shaykh (Rahimahu Allaah) hakutaja misingi hii kutoka kwake mwenyewe au kutoka kichwani mwake kama wanavyofanya wengi wanaochanganya mambo. Bali ameitoa misingi hii kutoka katika Kitabu cha Allaah na Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na historia yake.

Ukiitambua misingi hii na kuifahamu vyema, basi itakusahilikia baada ya hapo ni aina ipi ya Tawhiyd ambayo Allaah amewatuma kwayo Mitume Yake na akateremsha vitabu Vyake. Vilevile utaitambua shirki ambayo Allaah ametahadharisha nayo na akabainisha ukhatari na madhara yake duniani na Aakhirah. Jambo hili ni muhimu sana. Hili ni lazima kwako zaidi kuliko kuzijua hukumu zinazohusiana na swalah, zakaah, ´ibaadah mbalimbali na mambo mengine ya dini. Hili ndilo jambo la kwanza na la msingi, kwa sababu si swalah, zakaah, swawm, hajj na ´ibaadah nyenginezo hazisihi iwapo hazitojengwa juu ya ´Aqiydah sahihi, jambo ambalo ni kumpwekesha Allaah (´Azza wa Jall) kwa kumwabudu Yeye peke yake.

Hakika (Rahimahu Allaah) ameitangulizia misingi hii minne utangulizi mkubwa. Ndani yake mna kumuombea du´aa mwanafunzi na kumzindua kwa yale atayoyasema pale aliposema:

“Ninamuomba Allaah Mkarimu, Mola wa ´Arshi tukufu, akuhifadhi duniani na Aakhirah na akufanye ni mbarikiwa popote utapokuwa. Vilevile akufanye kuwa ni miongoni mwa wale wanapopewa basi hushukuru, wanapopewa mtihani basi husubiri na wanapotenda dhambi huomba msamaha. Hakika mambo haya matatu ndio ufunguo wa furaha.”

Katika utangulizi huu mkubwa Shaykh (Rahimahu Allaah) anamuombea kila mwanafunzi ambaye anaisoma ´Aqiydah yake kwa ajili ya kuifikia haki na kuepuka upotevu na shirki, kwa sababu mtu kama huyu ana haki zaidi kwa Allaah kumlinda duniani na Aakhirah. Yule ambaye Allaah atamlinda duniani na Aakhirah, basi hatoguswa na yenye kumchukiza si hapa duniani wala huko Aakhirah. Amesema (Ta´ala):

اللَّـهُ وَلِيُّ الَّذِينَ آمَنُوا يُخْرِجُهُم مِّنَ الظُّلُمَاتِ إِلَى النُّورِ ۖ وَالَّذِينَ كَفَرُوا أَوْلِيَاؤُهُمُ الطَّاغُوتُ

“Allaah ni mlinzi wa wale walioamini anawatoa kutoka katika viza na kuwaingiza katika nuru. Wale waliokufuru walinzi wao ni mashetani.” (02:257)

Allaah akikulinda, basi atakutoa kutoka katika viza, kama viza vya shirki, kufuru, mashaka na viza vya ukafiri na badala yake kukuingiza katika nuru ya imani, elimu yenye manufaa na matendo mema:

ذَٰلِكَ بِأَنَّ اللَّـهَ مَوْلَى الَّذِينَ آمَنُوا وَأَنَّ الْكَافِرِينَ لَا مَوْلَىٰ لَهُمْ

“Hivyo ni kwa kuwa Allaah ni mlinzi wa wale walioamini na kwamba makafiri hawana mlinzi.” (47:11)

Allaah akikulinda kwa ulinzi Wake, mafanikio Yake na uongofu Wake hapa duniani na huko Aakhirah, basi utafurahi furaha ambayo hutohisi mahuzuniko hata siku moja. Katika dunia hii atakulinda kwa uongofu, mafanikio na kupita juu ya mfumo uliosalimika. Aakhirah atakulinda kwa kukuingiza kwenye Pepo Yake ambapo utakuja kudumu humo milele. Humo hutohisi khofu, kupatwa na maradhi, kuhisi mahuzuniko, kuhisi dhiki wala kupatwa na yenye kuchukiza. Hivi ndivyo Allaah anavyomuhifadhi mja Wake muumini duniani na Aakhirah.

Maneno yake mtunzi:

“… na akufanye ni mbarikiwa popote utapokuwa… “

Lengo kubwa ni Allaah kukufanya kuwa ni mwenye kubarikiwa popote utapokuwa. Allaah anakujaalia kuwa ni mwenye kubarikiwa katika maisha yako, riziki yako, elimu yako, matendo yako na kizazi chako. Baraka zinakuandama popote unapokuwa na kuelekea. Hii ni kheri kubwa kabisa na fadhilah kutoka kwa Allaah (´Azza wa Jall).

Maneno yake mtunzi:

“… Vilevile akufanye kuwa ni miongoni mwa wale wanapopewa hushukuru… “

Tofauti na yule anayekufuru na kujivuna pale anapopewa neema. Hakika watu wengi wanapotunukiwa neema wanaikufuru. Aidha wanaikana na wanaitumia katika kusikokuwa kumtii Allaah (´Azza wa Jall). Hii bila ya shaka inakuwa ni sababu ya kuangamia kwao. Ama kuhusu yule mwenye kushukuru, basi Allaah humzidishia:

وَإِذْ تَأَذَّنَ رَبُّكُمْ لَئِن شَكَرْتُمْ لَأَزِيدَنَّكُمْ

“Pindi alipotangaza Mola wenu: “Ikiwa mtashukuru, bila hakika nitakuzidishieni.”” (14:07)

Allaah (´Azza wa Jall) huwazidishia wale wenye kushukuru kutokana na fadhilah na wema Wake. Kwa ajili hiyo ikiwa unataka kupewa neema zaidi, basi mshukuru Allaah (´Azza wa Jall) na kama unataka kuiondosha neema, basi ikufuru.

Maneno yake mtunzi:

“… wanapopewa mtihani basi husubiri… “

Allaah (Jalla wa ´Alaa) huwapa mitihani waja Wake. Huwapa mtihani wa misiba, yenye kuchukiza na maadui katika makafiri na wanafiki. Katika mnasaba huu wanahitajia kuwa na subira, kutokata tamaa na kutokatika moyo na huruma ya Allaah. Wanatakiwa kuwa na uthabiti katika dini yao na wasitikiswe na mitihani au wakajisalimisha nayo. Ni lazima kwao wawe imara katika dini yao na wastahamili zile tabu wanazokumbana nazo. Wasiwe kama wale ambao wanapopewa mtihani basi wanavunjika moyo, wanakasirika na wanakata tamaa na rehema za Allaah (´Azza wa Jall). Haya yanapelekea mitihani juu ya mitihani mingine na majanga juu ya majanga mengine. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Allaah anapowapenda watu basi huwapa mtihani. Ambaye ataridhia, basi hupata radhi na atayekasirika, basi hupatwa na hasira.”[1]

“Mitume ndio watu wenye kutiwa kwenye mitihani mikali. Halafu wale wenye kufanana na wao halafu wale wenye kufanana na wao.”[2]

Mitume walipewa mitihani, wakweli walipewa mitihani, mashahidi walipewa mitihani na waja wa Allaah waumini walipewa mitihani. Hata hivyo walisubiri. Lakini wanafiki Allaah (Ta´ala) amesema juu yao:

وَمِنَ النَّاسِ مَن يَعْبُدُ اللَّـهَ عَلَىٰ حَرْفٍ

“Miongoni mwa watu yuko yule anayemwabudu Allaah kwenye ncha… “

Bi maana kandokando.

فَإِنْ أَصَابَهُ خَيْرٌ اطْمَأَنَّ بِهِ ۖ وَإِنْ أَصَابَتْهُ فِتْنَةٌ انقَلَبَ عَلَىٰ وَجْهِهِ خَسِرَ الدُّنْيَا وَالْآخِرَةَ ۚ ذَٰلِكَ هُوَ الْخُسْرَانُ الْمُبِينُ

“… inapompata kheri, basi hupata matumaini kwayo, na anapofikwa na mitihani basi hugeuka nyuma juu ya uso wake; amekhasirika duniani na Aakhirah – hiyo ndiyo khasara ya wazi.” (22:11)

Dunia hii sio makazi ya kuneemeka, anasa, ladha, kufurahi na kushinda siku zote. Mambo hayako hivo siku zote. Allaah hubadilishabadilisha zamu kati ya waja Wake. Maswahabah, ambao ni watu bora wa Ummah, walikutana na majaribio na mitihani yepi? Amesema (Ta´ala):

وَتِلْكَ الْأَيَّامُ نُدَاوِلُهَا بَيْنَ النَّاسِ

“Na hizo ni siku Tunazizungusha zamu kati ya watu.” (03:140)

Kwa hiyo mja anatakiwa kujipoza kwa kutambua kwamba sio yeye peke yake aliyepewa majaribio. Haya tayari yameshatangulia kuwakuta vipenzi wa Allaah. Kwa ajili hiyo anatakiwa kujipoza nafsi yake, kusubiri na kusubiria faraja kutoka kwa Allaah (Ta´ala) – mwisho mwema ni wa wale wamchao Allaah.

Maneno yake mtunzi:

“… wanapotenda dhambi huomba msamaha.”

Ama yule ambaye anapotenda dhambi haombi msamaha na bali anaendelea kuzama katika dhambi, huyu ni mla khasara. Lakini mja muumini kila pale anapofanya dhambi, basi anakimbilia kuomba msamaha:

وَالَّذِينَ إِذَا فَعَلُوا فَاحِشَةً أَوْ ظَلَمُوا أَنفُسَهُمْ ذَكَرُوا اللَّـهَ فَاسْتَغْفَرُوا لِذُنُوبِهِمْ وَمَن يَغْفِرُ الذُّنُوبَ إِلَّا اللَّـهُ

“Na wale ambao wanapofanya machafu au wakajidhulumu nafsi zao, basi humdhukuru Allaah wakaomba msamaha kwa madhambi yao na nani anayesamehe madhambi isipokuwa Allaah?” (03:135)

إِنَّمَا التَّوْبَةُ عَلَى اللَّـهِ لِلَّذِينَ يَعْمَلُونَ السُّوءَ بِجَهَالَةٍ ثُمَّ يَتُوبُونَ مِن قَرِيبٍ

“Hakika si vyengienvyo tawbah inayokubaliwa na Allaah ni ya wale wanaofanya uovu kwa ujahili kisha wakatubia upesi.” (04:17)

Neno “ujahili” haina maana ya ujinga unaofahamika, kwa sababu mjinga haadhibiwi, bali ni kinyume cha “upole”. Kila mwenye kumuasi Allaah ni mjinga ambaye yuko na mpungufu wa upole, akili pungufu na uanaadamu mpungufu. Mtu anaweza kuwa mwanachuoni na wakati huohuo akawa ni mjinga kwa njia ya kwamba anakuwa hana upole na uimara katika mambo:

ثُمَّ يَتُوبُونَ مِن قَرِيبٍ

“… kisha wakatubia upesi.”

Hii ina maana ya kwamba kila wanapofanya dhambi, basi wanaomba msamaha. Hakuna yeyote ambaye amekingwa na dhambi, lakini himdi zote ni za Allaah kuona amefungua milango ya tawbah. Kwa ajili hiyo mja kila pale anapokosea anatakiwa kukimbilia kutubia. Lakini endapo hatotubia na kutaka msamaha, hii ni alama ya kula khasara. Mtu huyu kuna khatari akakata tamaa na huruma ya Allaah au shaytwaan akamjia na kumwambia: “Wewe huna tawbah.”

Mambo haya matatu ndio ufunguo wa furaha; anapopewa hushukuru, anapopewa mtihani husubiri na anapotenda dhambi anaomba msamaha. Yule atakayepewa nayo basi atapata furaha. Yule atayenyimwa mambo haya, au kimoja wapo, huyu ni mla khasara.

[1] at-Tirmidhiy (04/601) na Ibn Maajah (4031). at-Tirmidhiy amesema: “Hadiyth hii ni geni.” Vilevile imepokelewa na Ahamd (04/428).

[2] at-Tirmidhiy (07/131), al-Haakim (01/41) na al-Bayhaqiy (03/372). at-Tirmidhiy amesema: “Hadiyth hii ni nzuri na Swahiyh.”

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Qawaa´id al-Arba´ah, uk. 07-12
  • Imechapishwa: 18/08/2022