01. Sura ya kwanza: Maana ya ´Aqiydah na ubainifu juu ya umuhimu wake


´Aqiydah limetokamana na neno ufungaji. Ni kule kukifunga kitu. Mtu anaposema kuwa ameitakidi namna fulani anamaanisha kwamba ameifungamanisha juu yake moyo na dhamira. ´Aqiydah ni yale anayoamini mtu. Husemwa kwamba mtu ana ´Aqiydah nzuri bi maana iliyosalimika kutokamana na shaka.

´Aqiydah ni kitendo cha kimoyo. Ni kule moyo kuamini kitu na kukisadikisha.

´Aqiydah Kishari´ah maana yake ni kule kumwamini Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Yake, siku ya Mwisho na Qadar kheri na shari yake. Hizi huitwa vilevile kuwa ni nguzo za imani.

Shari´ah imegawanyika mafungu mawili:

1- Mambo ya kiitikadi.

2- Mambo ya kimatendo.

Mambo ya kiitikadi ni yale yasiyofungamana na namna ya matendo. Kama mfano wa kuamini uola wa Allaah, ulazima wa kumwabudu Yeye na kuamini nguzo zilizobaki za imani zilizotajwa. Huitwa vilevile ´mambo ya kimsingi`.

Mambo ya kimatendo ni yale yanayohusiana na namna ya matendo. Kama mfano wa swalah, zakaah, swawm na hukumu nyenginezo za kimatendo. Huitwa vilevile ´matawi `. Kwa sababu yamejengeka juu ya jambo hilo ima kwa kusihi na kuharibika[1].

´Aqiydah sahihi ndio msingi ambao dini inasimama juu yake na kwayo matendo yanapata kusihi. Amesema (Ta´ala):

فَمَن كَانَ يَرْجُو لِقَاء رَبِّهِ فَلْيَعْمَلْ عَمَلًا صَالِحًا وَلَا يُشْرِكْ بِعِبَادَةِ رَبِّهِ أَحَدًا

“Hivyo basi yule anayetaraji kukutana na Mola wake basi na atende matendo mema na wala asishirikishe katika ‘ibaadah za Mola wake yeyote!”[2]

وَلَقَدْ أُوحِيَ إِلَيْكَ وَإِلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكَ لَئِنْ أَشْرَكْتَ لَيَحْبَطَنَّ عَمَلُكَ وَلَتَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ

“Hakika umefunuliwa Wahy na kwa wale walio kabla yako kwamba: “Ukifanya shirki bila shaka yataporomoka matendo yako na hakika utakuwa miongoni mwa waliokhasirika.”[3]

فَاعْبُدِ اللَّـهَ مُخْلِصًا لَّهُ الدِّينَ أَلَا لِلَّـهِ الدِّينُ الْخَالِصُ

“Basi mwabudu Allaah kwa  kumtakasia dini Yeye. Tanabahi! Ni ya Allaah Pekee Dini iliyotakasika.”[4]

Aayah hizi tukufu na nyenginezo zilizokuja zikiwa na maana yake – nazo ni nyingi – zinafahamisha kuwa matendo hayakubaliwi isipokuwa pale ambapo yatakuwa yametakasika kutokamana na shirki. Kwa ajili hii ndio maana Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) walikuwa wakitilia umuhimu kuitengeneza ´Aqiydah kwanza. Kitu cha kwanza walikuwa wakiwalingania watu wao ni kumuabudu Allaah pekee na kutoabudu vyengine. Amesema (Ta´ala):

وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِي كُلِّ أُمَّةٍ رَّسُولًا أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ وَاجْتَنِبُوا الطَّاغُوتَ

”Hakika Tulituma katika kila ummah Mtume kwamba: “Mwabuduni Allaah na jiepusheni na Twaaghuut [waungu batili].”[5]

Kitu cha kwanza ambacho kila Mtume alikuwa akiwalingania kwacho watu wao ni:

اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ

“Enyi watu wangu! Mwabuduni Allaah, kwani hakika hamna mwabudiwa wa haki mwingine asiyekuwa Yeye.”[6]

اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ

“Enyi watu wangu! Mwabuduni Allaah, kwani hakika hamna mwabudiwa wa haki mwingine asiyekuwa Yeye.”[7]

اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ

“Enyi watu wangu! Mwabuduni Allaah, kwani hakika hamna mwabudiwa wa haki mwingine asiyekuwa Yeye.”[8]

اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ

“Enyi watu wangu! Mwabuduni Allaah, kwani hakika hamna mwabudiwa wa haki mwingine asiyekuwa Yeye.”[9]

Haya yalisemwa na Nuuh, Huud, Swaalih, Shu´ayb na Mitume wengine wote (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) kuwaambia watu wao.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam), baada ya kupewa utume, alibaki Makkah miaka kumi na tatu akiwalingania watu katika Tawhiyd na ´Aqiydah sahih. ´Aqiydah sahihi ndio msingi ambao dini inajengwa juu yake. Walinganizi na watengenezaji walikuwa ni mfano katika hili kwa kuwaiga Mitume na Manabii. Walikuwa wakianza kulingania katika Tawhiyd na kuirekebisha ´Aqiydah. Halafu baada ya hapo wanaelekea katika mambo mengine ya dini.

[1] Sharh ´Aqiydah as-Safaariyniyyah (01/04).

[2] 18:110

[3] 39:65

[4] 39:02-03

[5] 16:36

[6] 07:59

[7] 07:65

[8] 07:73

[9] 07:85

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 06-07
  • Imechapishwa: 13/01/2020