01. Sunnah iliyokokotezwa


Miongoni mwa mambo aliyoweka katika Shari´ah Mtume wa uongofu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika mwezi wa Ramadhaan ni swalah ya Tarawiyh. Ni Sunnah iliyokokotezwa. Imeitwa Tarawiyh(mapumziko) kwa sababu watu walikuwa wakipumzika ndani yake kati ya kila Rak´ah nne[1]. Kwa sababu walikuwa wakirefusha swalah.

Bora iswaliwe na kikosi cha watu msikitini. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwaswalisha Maswahabah zake msikitini nyusiku kadhaa. Kisha akaacha kufanya hivo kwa kuchelea isije kufaradhishwa juu yao. Hayo yamethibiti kwa al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Usiku mmoja Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliswali msikitini na watu kadhaa wakaswali pamoja naye. Kisha akaswali siku ya kufuata na watu wakawa wengi. Kisha wakakusanyika katika usiku wa tatu au wa nne na hakuwatokea. Kulipopambazuka akasema: “Nimeona mlichokifanya. Hakuna kilichonizuia kukutokeeni isipokuwa mimi nilichelea isije kufaradhishwa juu yenu.”[2]

Wakati huo ilikuwa katika Ramadhaan. Ikaswaliwa na Maswahabah baada yake na ummah wakaipokea kwa mikono miwili.

[1] Kati ya kila Tasliym mbili. Kwa sababu swalah ya Tarawiyh ni Rak´ah mbilimbili na vivyo hivyo juu ya swalah ya Tahajjud. Wakati mwingine hukosea baadhi ya maimamu wa misikiti ambao hawana uelewa. Utawaona hawatoi salamu baina ya kila Rak´ah mbili katika Tarawiyh na Tahajjud, kitu ambacho kinakwenda kinyume na Sunnah.

Wanazuoni wamesema kuwa ambaye atasimama kwenye Rak´ah ya tatu katika Tarawiyh au katika Tahajjud ni kama ambaye anasimama katika Rak´ah ya tatu kwenye Fajr. Kwa msemo mwingine ni kwamba swalah yake inabatilika. Shaykh ´Abdul-´Aziyz bin Baaz analo jawabu ambalo amewaraddi watu hawa na kubainisha kosa lao.

[2] al-Bukhaariy (1129) na Muslim (1780).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Mulakhasw al-Fiqh (01/167-168)
  • Imechapishwa: 05/05/2021