01. Sifa hizi zinapasa kuaminiwa kama zilivyokuja

Namwomba Allaah mafanikio na kusema:

Ni jambo la haramu juu ya akili kumfananisha Allaah, juu ya fikira kumfanyia kikomo na juu ya busara kumsifu isipokuwa vile Alivyojisifia Mwenyewe au vile Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alivyomsifu.

Ni jambo limesihi kutoka kwa Ahl-us-Sunnah wote mpaka hii leo kwamba khabari zote zilizothibiti kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) basi ni lazima kwa muislamu kuziamini kama zilivyopokelewa na kujua kwamba ni Bid´ah kuulizia maana yake na ukafiri na uzandiki kujibu. Mfano wake ni maneno Yake (Ta´ala):

هَلْ يَنظُرُونَ إِلَّا أَن يَأْتِيَهُمُ اللَّـهُ فِي ظُلَلٍ مِّنَ الْغَمَامِ وَالْمَلَائِكَةُ

“Je, wanangojea nini isipokuwa Allaah awajie katika vivuli vya mawingu pamoja na Malaika?”[1]

الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ

“Mwingi wa huruma amelingana juu ya ‘Arshi.”[2]

وَجَاءَ رَبُّكَ وَالْمَلَكُ صَفًّا صَفًّا

“Atakapokuja Mola wako na Malaika safu kwa safu.”[3]

Pia mfano wake yale yaliyozungumzwa na Qur-aan kama mfano wa ujuu, nafsi, mikono, usikizi, uoni, maneno, macho, kuonekana, matakwa, kuridhika, ghadhabu, mapenzi, kuchukia, uangalizi, ukaribu, umbali na kustahi.

Vivyo hivyo kusogea kiasi cha umbali wa mapinde mawili au karibu zaidi, kupanda kwa neno zuri Kwake, Malaika na Roho kupanda Kwake na kushuka kwa Qur-aan.

Kadhalika kuwaita Kwake Mitume kwa sauti, maneno Yake kwa Malaika, kukamata Kwake, kukunjua Kwake, ujuzi Wake, upwekekaji Wake, utashi Wake, kukusudiwa Kwake kwa haja zote na umoja Wake.

Vivyo hivyo kuhusu kwamba Yeye ndiye wa Kwanza, wa Mwisho, Aliye dhahiri na Aliyejificha.

Kadhalika inahusu Uhai Wake na kubaki Kwake milele, umilele Wake na kudumu Kwake, nuru Yake na kujionyesha Kwake, uso na haki, muundi na kumuumba Kwake Aadam kwa mikono Yake. Sifa na shukurani, njama, kushinda na asiyepingika. Vivyo hivyo inahusu maneno Yake:

أَأَمِنتُم مَّن فِي السَّمَاءِ أَن يَخْسِفَ بِكُمُ الْأَرْضَ فَإِذَا هِيَ تَمُورُ أَمْ أَمِنتُم مَّن فِي السَّمَاءِ أَن يُرْسِلَ عَلَيْكُمْ حَاصِبًا ۖ فَسَتَعْلَمُونَ كَيْفَ نَذِيرِ

“Je, mnadhani mko katika amani na aliyeko juu mbinguni kwamba hatokudidimizeni ardhini, tahamaki hiyo inatikisika? Au mnadhani mko katika amani na aliyeko juu mbinguni kwamba hatokutumieni tufani ya mawe basi mtajua vipi maonyo Yangu.”[4]

وَهُوَ الَّذِي فِي السَّمَاءِ إِلَـٰهٌ وَفِي الْأَرْضِ إِلَـٰهٌ ۚ وَهُوَ الْحَكِيمُ الْعَلِيمُ

”Yeye ndiye Mungu wa haki mbinguni na Mungu wa haki ardhini pia. Naye ndiye Mwenye hekima ya kila kitu, Mjuzi wa yote.”[5]

Allaah amewasikia wengine na kuna ambao wamemsikia Allaah. Pia sifa nyenginezo zilizofungamana Naye na zimetajwa katika Kitabu Chake zilizoteremshwa kwa Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

[1] 2:210

[2] 20:5

[3] 89:22

[4] 67:16-17

[5] 43:84

  • Mhusika: Imaam Abul-Qaasim Sa´d bin ´Aliy bin Muhammad az-Zinjaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ajwibah fiy Usuul-id-Diyn, uk. 54-65
  • Imechapishwa: 10/06/2021