01. Shirki ya waziwazi na shirki iliojificha

Shaykh (Rahimahu Allaah) ametaja mlango huu ili kubainisha yale makemeo yaliyokuja kuhusu kujionyesha na kuonyesha kuwa ni shirki inayoharibu kitendo kilichochanganyikana nayo. Mlango huu umetajwa ndani ya Kitaab-ut-Tawhiyd kwa sababu umetaja aina fulani ya shirki ndogo. Shaykh (Rahimahu Allaah) ametunga kitabu hiki kwa ajili ya kubainisha Tawhiyd na kubainisha shirki kubwa inayoivunja na shirki ndogo inayoipunguza.

Kuna shirki ilio waziwazi inayoonekana na kuna shirki yenye kujificha. Shirki inayoonekana ni ile inayokuwa katika matendo yenye kuonekana kama mfano wa kuchinja kwa ajili ya mwengine asiyekuwa Allaah, kumuwekea nadhiri asiyekuwa Allaah, kumtaka msaada asiyekuwa Allaah na mengineyo katika shirki kubwa ambayo inaonekana na kusikika na watu.

Shirki aina ya pili ni ile yenye kujificha. Hii watu hawawezi kuihisi wala kuiona, kwa sababu inakuwa ndani ya mioyo.

Shirki yenye kuonekana inakuwa katika yale matendo ya waziwazi. Jambo hili inapokuja katika nia na makusudio ya kimoyo ni mambo ambayo hakuna awezaye kuyajua isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Kwa ajili hiyo ndio maana Shaykh (Rahimahu Allaah) akataja mlango huu.

Mifano yote iliotangulia juu ya aina mbalimbali za shirki zinahusiana na shirki yenye kuonekana. Kwa ajili hiyo ´Allaamah Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) amesema:

Jichunge na shirki
kuna shirki yenye kuonekana
imegawanyika na haisameheki
Ni kule kumfanyia mshirika Mwingi wa huruma
pasi na kujali kama ni jiwe au mtu
anayeombwa, akatarajiwa, akaogopwa na kupendwa
kama anavyopendwa Allaah

Kuabudu masanamu, makaburi, miti na mawe yote haya ni shirki ya waziwazi.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: I´aanat-ul-Mustafiyd bi Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 439
  • Imechapishwa: 16/08/2019