Tawhiyd ndio msingi maisha ya mwanadamu, shirki ni kitu kulichojitokeza. Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

”Baina ya Aadam na Nuuh kulipita karne kumi. Wote walikuwa wakimwabudu Allaah pekee.”

 Shirki ilianza kujitokeza kwa watu wa Nuuh wakati walipochupa mipaka kwa waja wema na wakatengeneza picha zao. Matokeo yake wakawaabudu badala ya Allaah. Ndipo Allaah akamtuma Mtume wake Nuuh (´alayhis-Salaam) awakataze shirki na awaamrishe kumwabudu Allaah pekee asiyekuwa na mshirika. Mitume wengine wote baada yake wakaja na mtindo huohuo. Amesema (Ta´ala):

وَمَا أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ مِن رَّسُولٍ إِلَّا نُوحِي إِلَيْهِ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنَا فَاعْبُدُونِ

“Hatukutuma kabla yako Mtume yeyote isipokuwa Tulimfunulia Wahy ya kwamba: “Hakika hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Mimi; hivyo basi niabuduni.”[1]

Shirki kwa watu wa Muusa (´alayhis-Salaam) ilijitokeza wakati walipomwabudu ndama. Allaah katika Kitabu Chake ameeleza msimamo aliochukua Muusa na nduguye Haaruun (´alayhimaas-Salaam).

Shirki kwa manaswara ilitokea baada ya al-Masiyh (´alayhis-Salaam) kupandishwa juu mbinguni. Ilitokea mikononi mwa myahudi kwa jina Paulo. Alidhihirisha kumwamini al-Masiyh kwa ajili ya njama na udanganyifu. Matokeo yake akaingiza ndani ya dini ya unaswara imani ya utatu, kuabudu msalaba na mengine mengi ya kikafiri.

Shirki katika kizazi cha Ismaa´iyl, bi maana waarabu, ilijitokeza mikononi mwa ´Amr bin Luhayy al-Khuzaa´iy. Yeye ndiye alibadilisha dini ya Ibraahiym (´alayhis-Salaam), akayaleta masanamu Hijaaz na akawaamrisha watu wayaabudu.

Kuhusiana na shirki kwa baadhi ya waislamu, ilijitokeza kupitia Shiy´ah Faatwimiyyah baada ya karne ya nne. Ilikuwa pindi walipoanza kujenga juu ya makaburi, wakazusha Bid´ah ya mazazi ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wakawa na msimamo wa kuchupa mipaka kwa watu wema. Kadhalika wakati kulipojitokeza Taswawwuf zenye kupinda zilizoambatana na misimamo ya kuchupa mipaka kwa Mashaykh na watu wa twariqa.

Pamoja na haya yote Allaah amechukua dhamana ya kuilinda dini hii baada ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kupitia wanachuoni wenye kutengeneza na walinganizi wenye kujadidi ambao Allaah anawatuma kila kunapotimia miaka mia moja. Ndio maana haki siku zote imeendelea kubaki kuwa juu na dini wenye kuihami. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakutoacha kuendelea kuwepo kikundi kutoka katika Ummah wangu kuwa ni chenye kushinda juu ya haki. Hakitodhurika na wale wenye kuwakosesha nusura wala kwenda kinyume nao mpaka ije amri ya Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) ilihali wako katika hali hiyohiyo.”[2]

[1] 21:25

[2] al-Bukhaariy (7311), Muslim (4951) na Ahmad (18135).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: I´aanat-ul-Mustafiyd bi Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 05-10