01. Salaf walikemea na wakatahadharisha Bid´ah

Himdi zote njema anastahiki Allaah ambaye ametukamilishia dini na akatutimizia nema. Swalah na amani zimwendee Nabii na Mtume Wake Muhammad, ambaye ni Nabii wa tawbah na rehema.

Amma ba´d:

Allaah (Ta´ala) amesema:

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا

 “Leo wamekata tamaa wale waliokufuru juu ya dini yenu, hivyo basi msiwaogope na niogopeni Mimi. Leo nimekukamilishieni dini yenu na nimekutimizieni neema Yangu na nimekuridhieni Uislamu uwe dini yenu.”[1]

أَمْ لَهُمْ شُرَكَاءُ شَرَعُوا لَهُم مِّنَ الدِّينِ مَا لَمْ يَأْذَن بِهِ اللَّـهُ ۚ وَلَوْلَا كَلِمَةُ الْفَصْلِ لَقُضِيَ بَيْنَهُمْ ۗ وَإِنَّ الظَّالِمِينَ لَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ

“Je, wanao washirika waliowaamuru dini yale ambayo Allaah Hakuyatolea kwayo idhini? Na lau si neno la uamuzi [ulokwishapita], bila shaka ingelikidhiwa baina yao; na hakika madhalimu watapata adhabu iumizayo.”[2]

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Yeyote atakayezua katika amri yetu hii yale yasiyokuwemo basi atarudishiwa.”[3]

Imekuja katika tamko la Muslim:

“Yeyote akayefanya kitendo ambacho hamna ndani yake dini yetu atarudishiwa.”

Katika “as-Swahiyh” ya Muslim amepokea kupitia kwa Jaabir (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akisema katika Khutbah siku ya ijumaa:

“Amma ba´d; hakika mazungumzo bora ni Kitabu cha Allaah na uongofu bora ni wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Uovu wa mambo ni yale yaliyozuliwa. Kila Bid´ah ni upotofu.”[4]

Aayah na Hadiyth zilizo na maana kama hiyo ni nyingi ambazo zinajulisha dalili ya wazi kabisa ya kwamba Allaah ameukamilishia Ummah huu dini yake, akaitimiza neema yake na wala hakufa Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) isipokuwa baada ya kufikisha ufikishaji wa wazi na akaubainishia Ummah yale maneno na matendo ambayo Allaah amewawekea katika Shari´ah. Ameweka wazi (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba yale maneno na matendo yote yanayoelezwa na watu baada yake na wakayanasibisha katika dini ya Uislamu yote ni Bid´ah na yanayorudishwa kwa yule mwenye kuyazua ijapo mwenye nayo ana nia nzuri. Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walilitambua jambo hilo na vivyo hivyo wanazuoni wa Uislamu baada  yao. Hivyo walikemea na wakatahadharisha Bid´ah. Hayo yametajwa na kila ambaye ametunga katika kuadhimisha Sunnah na kukemea Bid´ah. Mfano wa watu hao ni Ibn Wadhdhwaah, at-Twurtwuushiy, Abu Shaamah na wengineo.

[1] 05:03

[2] 42:21

[3] al-Bukhaariy (2550) na Muslim (1718).

[4] Muslim (867).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tahdhiyr minal-Bid´ah, uk. 21-22
  • Imechapishwa: 16/01/2022