01. Ni kwa kitu gani inawajibika funga ya Ramadhaan?

Funga ya Ramadhaan inawajibika kwa moja ya mambo mawili na hakuna la tatu:

La kwanza: Kwa kuuona mwezi  mwandamo wa Ramadhaan.

La pili: Kukamilisha Sha´baan siku thelathini.

Ni lazima vilevile kufungua Ramadhaan kwa moja ya mambo mawili na hakuna la tatu:

La kwanza: Kwa kuuona mwezi wa Shawwaal.

La pili: Kukamilisha Ramadhaan siku thelathini kukithibiti kuuona mwezi wa Ramadhaan kwa ushahidi wa watu wa wawili waadilifu.

Dalili juu ya hayo ni nyingi katika Sunnah takasifu. Miongoni mwazo ni yale yaliyothibiti kwa al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa ´Abdullaah bin ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambaye amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Msifunge mpaka muuone mwezi mwandamo na wala msifungue mpaka muuone. Mkizuiwa na mawingu basi kadirieni.”[1]

Katika tamko la al-Bukhaariy imekuja:

”Mmwezi una nyusiku ishirini na tisa. Msifunge mpaka muuone. Endapo mtazuiwa na mawingu basi kamilisheni idadi ya siku thelathini.”[2]

Katika Hadiyth ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) kwa Muslim imekuja:

”Mkifunikwa na mwezi basi fanyeni siku thelathini.”

Wanachuoni wengi wanaona kuwa makussudio ya maneno yake:

”… basi kadirieni.”

ni kutazama mwanzoni mwa mwezi na kuhesabu hali ya kukamilisha siku thelathini. Tafsiri hii inatiliwa nguvu na mapokezi yaliyokuja kusema hivo kwa uwazi. Kitu kingine kinanchotilia nguvu maana hii ni zile Hadiyth zilizopokelewa ambazo zimekataza kufunga sik ya shaka kama mfano wa Hadiyth ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesimuliwa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mmoja wenu asiitangulizie Ramadhaan kwa kufunga siku moja au mbili. Isipokuwa mtu ambaye alikuwa akifunga swawm. Basi aiendeleze.”[3]

Vilevile Hadiyth ya ´Ammaar kwa al-Bukhaariy yenye mlolongo wa wapokezi uliopungua  hali ya kukata:

”Mwenye kufunga siku ya shaka basi amemuasi Abul-Qaasim (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”[4]

Kadhalika imethibiti kwa al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesimulia ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Sisi ni Ummah ummiyyah; hatuandiki wala hatuhesabu. Mwezi ni hivi na hivi.” yaani mara ishirini na tisa na mara thelathini.”[5]

Hadiyth hii ni dalili inayoonyesha ubatilifu wa kutegemea hesabu kuanza na kuisha kwa Ramadhaan. Kinachozingatiwa ni kuona mwezi au kukamilisha idadi ya siku thelathini. Hadiyth inausifu Ummah huu wa Kiislamu kwamba aghlabu yao kuandika na kuhesabu si jambo lao katika kuanza na kuisha kwa mwezi japokuwa ni wenye kuandika na kuhesabu katika mambo mengine kama mfano wa biashara na mengineyo. Makusudio ni kwamba hawategemei hesabu na bali wanategemea kuuona mwezi mwandamo katika hukumu. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amefungamanisha hukumu kwa kuuona mwezi na si kwa kuhesabu. Jambo la kuona linawezwa na msomi na asiyekuwa msomi, mjinga na mwanachuoni. Hii ni dalili inayothibitisha kuwa Shari´ah. Shukurani zote njema ni Zake kwa yale aliyofanya mepesi. Yeye ni Mwenye hekima kamilifu juu ya yale anayostahiki kuwawekea Shari´ah waja Wake kutokana na yale manufaa na rehema anazotambua (Subhaanah) juu yao. Kwani Yeye ni Mwingi wa hekima, mjuzi wa kila kitu (Subhaanah).

[1] al-Bukhaariy (1906) na Muslim (1080).

[2] al-Bukhaariy (1907).

[3] al-Bukhaariy (1914) na Muslim (1082).

[4] Ameipokea al-Bukhaariy ikiwa na cheni ya wapokezi uliopungua (03/27).

[5] al-Bukhaariy (1913) na Muslim (1080).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtaswaru fiy Ahkaam-is-Swiyaam, uk. 07-09
  • Imechapishwa: 10/04/2019