´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy (rahimahullaah) amesema:

Swali 1: Ni ipi tafsiri ya Tawhiyd? Vigawanyo vyake ni vingapi?

Jibu: Tafsiri ya Tawhiyd ya jumla iliokusanya aina zake zote ni:

Elimu ya mja, itikadi, kukiri na kuamini kwake kupwekeka kwa Allaah kwa kila sifa ya ukamilifu. Vilevile kuamini ya kwamba hakuna mshirika wala kitu kilicho na sehemu katika ukamilifu Wake. Hali kadhalika ina maana ya kwamba mtu aamini kuwa Yeye ndiye ana haki ya kuabudiwa na viumbe pasina kujali inahusiana na ´ibaadah aina gani.

Katika tafsiri hii kunaingia vigawanyo vitatu vya Tawhiyd:

1 – Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah: Kukiri ya kwamba Mola amepwekeka katika kuumba, kuruzuku, kuyaendesha mambo na kulea.

2 – Tawhiyd Asmaa´ was-Swifaat: Kuthibitisha yale yote ambayo Allaah amejithibitishia katika nafsi Yake Mwenyewe na ambayo amemthibitishia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) miongoni mwa majina mazuri na sifa kuu. Uthibitishaji huu unatakiwa kuwa pasi na kushabihisha na kufananisha na sifa za viumbe, pasi na kupotosha na kukanusha.

3 – Tawhiyd-ul-´Ibaadah: Ni mtu kumpwekesha na kumtakasia Allaah aina zote za ´ibaadah bila ya kumshirikisha katika chochote katika hayo.

Hivi ndivyo vigawanyo vya Tawhiyd. Mtu hawezi kuwa mpwekeshaji mpaka avitekeleze vyote.

MAELEZO

Tawhiyd maana yake ni kuamini upwekekaji wa Allaah kwa kila sifa kamilifu. Ana uwezo wa kutoshindwa chochote. Ana hekima kubwa ambayo kwayo anakiweka kila kitu mahali pake stahiki. Ana elimu ambayo imekizunguka kila kinachojulikana. Hakuna chochote kinachofichikana katika elimu Yake. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَخَلَقَ كُلَّ شَيْءٍ ۖ وَهُوَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ

“Ameumba kila kitu Naye juu ya kila jambo ni Mjuzi.”[1]

Allaah ndiye Muumbaji, Mwenye kuruzuku, Muweza na Mjuzi ambaye amekizunguka kila kitu kiujuzi. Allaah ndiye ambaye kamuumba mwanadamu na akamsahilishia riziki yake na akamdhibitia matendo yake. Allaah (Ta´ala) amesema:

مَّا يَلْفِظُ مِن قَوْلٍ إِلَّا لَدَيْهِ رَقِيبٌ عَتِيدٌ

“Hatamki yeyote neno isipokuwa anaye mchungaji aliyejitayarisha kuandika.”[2]

وَإِنَّ عَلَيْكُمْ لَحَافِظِينَ كِرَامًا كَاتِبِينَ

“Hakika juu yenu bila shaka kuna wenye kuhifadhi; watukufu wenye kuandika.”[3]

Allaah atamlipa kila mja kwa matendo yake. Ikiwa ni kheri, basi atamlipa kheri, na ikiwa ni shari, atamlipa shari. Anamwongoza yule Amtakaye katika matendo ya furaha kwa fadhilah Zake na anamkosesha nusura yule Amtakaye kwa uadilifu Wake. Anamiliki mbingu saba na vilivyomo ndani yake na anamiliki ardhi saba na vilivyomo ndani yake. Kwa hivyo mja akiitakidi imani hii na akatambua uola wa Mola Wake juu yake, basi hapo italazimika vilevile kumpwekesha kwenye matendo yake. Yule mwenye kukiri upwekekaji wa Mola Wake katika ´ibaadah basi itamlazimu vilevile kumwabudu Yeye pekee kwa mujibu wa Shari´ah ya Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam.

Tawhiyd imegawanyika katika mafungu matatu:

1 – Umpwekeshe kwa matendo Yake kama vile kuumba, kuruzuku na kuendesha mambo.

2 –  Umpwekeshe kwa majina na sifa Zake kama vile ujuzi, uwezo, usikizi, uoni na nyenginezo.

3 – Tumpwekeshe kwa matendo yetu. Nazo ni zile ´ibaadah ambazo Allaah ametuwajibishia nazo na akazifanya kuwa ndio sababu za kuokoka kwa yule mwenye kuzifanya, furaha yake na kufaulu kwake Pepo.

Kwa ufupi vigawanyo vya Tawhiyd ni kama ifuatavyo:

1 – Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah. Aina hii haimwingizi yeyote ndani ya Uislamu. Kwa sababu washirikina ambao walitumiliziwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walikuwa wakikubali aina hii, lakini haikuwafanya wakawa waislamu.

2 – Tawhiyd-us-Asmaa´ was-Swifaat. Aina hii mtu anatakiwa kuamini majina na sifa za Allaah kwa njia inayolingana na utukufu wa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

3 – Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah. Aina hii ndio kulitokea migogoro kati ya Mitume na nyumati zao.

[1] 06:101

[2] 50:18

[3] 82:10-11

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath Rabb-il-Bariyyaat ´alaa Kitaab Ahamm-il-Muhimmaat, uk. 17-20
  • Imechapishwa: 20/09/2021