01. Nasaha kabla ya hajj


Natanguliza nasaha na faida hizi kwa ndugu zangu mahujaji kabla ya hajj:

1- Ni wajibu kwa mwenye kufanya hajj kumcha Mola wake na apupie kwelikweli  kutotumbukia katika yale Allaah aliyomharamishia. Amesema (Ta´ala):

 الْحَجُّ أَشْهُرٌ مَّعْلُومَاتٌ ۚ فَمَن فَرَضَ فِيهِنَّ الْحَجَّ فَلَا رَفَثَ وَلَا فُسُوقَ وَلَا جِدَالَ فِي الْحَجِّ

“Hajj [inatakiwa kutekelezwa katika] miezi maalum. Yule ambaye imemfaradhikia [katika miezi hiyo kwa kupata uwezo wa kwenda] hajj basi asifanye jimaa, ufasiki wala mabishano.”[1]

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yule mwenye kuhiji na asifanye jimaa wala maneno machafu, basi anarudi kama siku alivozaliwa na mama yake.”

Endapo atafanya hivo basi hajj yake inakuwa ni yenye kukubaliwa. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hajj iliyokubaliwa haina malipo isipokuwa Pepo.”[2]

Kwa hivyo ni lazima kutahadhari na yale waliyopewa mtihani kwayo baadhi yao kwa sababu ya ujinga au upotevu wao:

a) Kumshirikisha Allaah. Tumewaona wengi wao wanatumbukia katika shirki. Kama vile kutaka uokozi kwa asiyekuwa Allaah. Wanawaomba msaada kwa Mitume ambao ni wafu na waja wema. Wanawaomba wao badala ya Allaah. Wanaapa kwao kwa ajili ya kuwaadhimisha. Kwa ajili hiyo wanazibatilisha hajj zao. Amesema (Ta´ala):

لَئِنْ أَشْرَكْتَ لَيَحْبَطَنَّ عَمَلُكَ

“Ukifanya shirki basi hakika yataporomoka matendo yako.”[3]

b) Baadhi yao hujipamba kwa kunyoa ndevu, jambo ambalo ni dhambi nzito. Kitendo hicho kina muhalafa nne, imetajwa katika “msingi”.

c) Wanaume huvaa pete ya dhahabu, jambo ambalo ni haramu. Uharamu unakuwa mkubwa zaidi ikiwa ni pete ya uchumba, jambo ambalo vilevile ni kujifananisha na manaswara.

2- Yule ambaye amekusudia kuhiji na akawa hana mnyama[4], basi ni wajibu wake anuie hajj ya Tamattu´ kwa sababu ndio ambayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwaamrisha Maswahabah zake mwishoni wa jambo. Kwa sababu vilevile ya kuwaghadhibikia kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) Maswahabah zake ambao hawakufanya haraka katika kutekeleza amri yake ya kuifisidi hajj kwa ajili ya ´Umrah. Amesema vilevile:

” ´Umrah imeingizwa kwenye hajj mpaka siku ya Qiyaamah.”

Wakati Maswahabah walipomuuliza kama hayo yanahusu mwaka huu peke yake au ni milele, ndipo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akapachanisha vidole vyake na kusema:

“Umilele. Umilele.”[5]

Kwa ajili hiyo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwamrisha Faatwimah na wakeze (Radhiya Allaahu ´anhunn) wajivue kutoka kwenye Ihraam baada ya kufanya ´Umrah ya hajj. Kwa ajili hiyo Ibn ´Abbaas alikuwa akisema:

“Atakayetufu kwenye Nyumba tukufu basi atakuwa ameshatoka kwenye Ihraam. Hiyo ndio Sunnah ya Mtume wenu hata kama mtachukia.”[6]

Ni kwa kila yule ambaye hakukokota kichinjwa anuie ´Umrah ndani ya miezi hii mitatu ya hajj. Yule ambaye ataleta Talbiyah ya hajj hali ya kuwa ni mwenye kufanya Ifraad na Qiraan kisha akafikiwa na amri ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kuivunja, basi anatakiwa kukimbilia hilo, hata kama ni baada ya kufika Makkah, kufanya Twawaaf na kutembea kati ya Swafaa na Marwah. Katika hali hii atoke kwenye Ihraam na anuie hajj yake kwenye Tarwiyah siku ya nane:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اسْتَجِيبُوا لِلَّـهِ وَلِلرَّسُولِ إِذَا دَعَاكُمْ لِمَا يُحْيِيكُمْ

“Enyi walioamini! Muitikieni Allaah na Mtume anapokuiteni katika yale yenye kukupeni uhai.”[7]

  3- Tahadhari kuacha kulala Minaa, katika ule usiku wa ´Arafah, kwa sababu ni wajibu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alifanya na kuamrisha hivo pale aliposema:

“Chukueni kutoka kwangu ´ibaadah zenu za hajj!”

Ni wajibu vilevile kulala Muzdalifah mpaka utaposwali swalah ya alfajiri. Kama kutakupita kulala pale, basi usipitwe kutekeleza swalah pale, kwa sababu hiyo ni wajibu zaidi. Bali ni nguzo miongoni mwa nguzo za hajj kwa mujibu wa wanachuoni wahakiki. Isipokuwa kwa wanawake na wanyonge. Inafaa kwa wao kuondoka sehemu hiyo baada ya nusu ya usiku.

4- Fanya uwezavyo usipite mbele ya yeyote mwenye kuswali katika msikiti Mtakatifu, sembuse misikiti mingine. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Lau atajua mwenye kupita mbele ya mwenye kuswali ni kitu gani kinachompatikania, basi ingelikuwa bora kwake kusimama arubaini kuliko kupita mbele yake.”

Maandiko haya ni yenye kuenea na yanamgusa kila mwenye kupita na kila mwenye kuswali. Isitoshe Hadiyth inayomvua yule mwenye kupita katika msikiti Mtakatifu haikusihi.

Ni wajibu kwako vilevile kuswali kuelekea Sutrah kama unavyofanya katika misikiti mingine yote kwa sababu ya kuenea Hadiyth zilizokuja juu ya jambo hilo. Kuna mapokezi maalum kutoka kwa baadhi ya Maswahabah juu ya jambo hili na yametajwa katika “msingi”.

5- Ni wajibu kwa wanachuoni na watu wenye fadhila kuwafundisha mahujaji ´ibaadah za hajj popote watapokutana nao na hukumu zake kwa mujibu wa Qur-aan na Sunnah. Hata hivyo lisiwashughulishe hilo kuacha kulingania katika Tawhiyd, amabyo ndio msingi wa Uislamu na kwa ajili yake wakatumwa Mitume na kukateremshwa Vitabu. Wengi katika ambao tumekutana nao – hata baadhi ya wale wanaojinasibisha na elimu – tumewakuta wako katika ujinga wa kupea juu ya uhakika wa Tawhiyd ya Allaah na sifa Zake. Kama vile ambavyo wako katika ughafilikaji uliokamilika kuhusiana na ulazima wa waislamu kuwa na umoja juu ya msingi wa Qur-aan na Sunnah katika ´Aqiydah, hukumu, matangamano, tabia, siasa, uchumi na mengineyo katika mambo ya kimaisha.

Wanatakiwa kukumbuka kwamba sauti yoyote itakayonyanyuliwa na isilahi yoyote itakayosimama juu ya isiyokuwa msingi na njia hii iliyonyooka, basi haitowafanya waislamu jengine isipokuwa kufarikiana na udhaifu, hizaya na utwevu. Uhalisia wa hali ilivyo ni ushahidi mkubwa juu ya hilo – Allaah ndiye mwenye kutakwa msaada.

Inafaa kujadiliana kwa njia iliyokuwa nzuri, kukiwa kuna haja ya kufanya hivo. Sampuli ya mjadala uliokatazwa katika hajj ni mjadala wa batili, ambao umekatazwa hata nje ya hajj pia. Vivyo hivyo inahusiana na madhambi. Haihusiani na sampuli ya mjadala ule ulioamrishwa kwa mfano katika maneno Yake (Ta´ala):

ادْعُ إِلَىٰ سَبِيلِ رَبِّكَ بِالْحِكْمَةِ وَالْمَوْعِظَةِ الْحَسَنَةِ ۖ وَجَادِلْهُم بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ

“Lingania katika njia ya Mola wako kwa hekima na mawaidha yaliyo mazuri, na jadiliana nao kwa ile nji iliyo nzuri zaidi.”[8]

Pamoja na hivyo inatakiwa kwa yule mwenye kujadili pale itampombainikia kuwa hakuna manufaa ya kujadiliana na wapinzani – ima kwa sababu ya ule ushabiki wake katika madhehebu au maoni yake au mjadala ule ukawa unapelekea katika mambo yasiyojuzu – hapo itakuwa ni bora kwake yeye kujiepusha na kujadiliana nao. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mimi ni mwenye kumdhamini nyumba katikati ya Pepo kwa yule mwenye kuacha ubishi hata kama yuko kwenye haki.”

[1] 02:197

[2] Ameipokea al-Bukhaariy, Muslim na wengineo kutoka kwa Hadiyth ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh). Imetajwa katika ”Silsilah al-Ahaadiyth as-Swahiyhah” (1200) na ”al-Irwaa’” (769).

[3] 39:65

[4] Hivyo ndivyo ilivyo hali ya mahujaji wengi hii leo. Ni mara chache mtu akakokota mnyama wake kutoka mahala palepale kama alivyofanya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mwenye kufanya hivo basi asikemewe. Ama kuhusu yule ambaye hakuja na mnyama wowote na badala yake akahiji Qiraan au Ifraad, basi kitendo chake kimeenda kinyume na kitendo na maamrisho yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), hata kama watu watapendelea kinyume. Haya yamesemwa na Ibn ´Abbaas na imepokelewa na Muslim (04/58) na Ahmad (01/287) na (01/342).

[5] Tazama ”Swahiyh Sunan Abiy Daawuud” (1568) na (1571).

[6] Yanatokamana na maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Allaah ameiingiza ´Umrah kwenye hajj yenu. Yule mwenye kufanya Twawaaf kwenye Nyumba na akatembea kati ya Swafaa na Marwah ametoka kwenye Ihraam isipokuwa yule ambaye hana kichinjwa.” (Tazama ”Swahiyh Sunan Abiy Daawuud (1573) na (1580))

[7] 08:24

[8] 16:125

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Manaasik-ul-Hajj wal-´Umrah, uk. 6-10
  • Imechapishwa: 13/08/2017