01. Nafasi ya Sunnah katika Qur-aan na ubainifu ya kwamba Qur-aan peke yake haitoshi

Himdi zote anastahiki Allaah. Tunamhimidi Yeye, kumuomba msaada na msamaha. Tunajilinda kwa Allaah kutokamana na shari ya nafsi zetu na uovu wa matendo yetu. Hakika yule mwenye kuongozwa na Allaah, basi hakuna wa kumpoteza, na yule mwenye kupotezwa na Allaah, basi hakuna wa kumwongoza. Nashuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah, hali ya kuwa ni Mmoja asiyekuwa na mshirika, na nashuhudia ya kwamba Muhammad ni mja na ni Mtume Wake.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ حَقَّ تُقَاتِهِ وَلَا تَمُوتُنَّ إِلَّا وَأَنتُم مُّسْلِمُونَ

“Enyi walioamini! Mcheni Allaah ukweli wa kumcha na wala msife isipokuwa nyinyi ni waislamu.” (03:102)

يَا أَيُّهَا النَّاسُ اتَّقُوا رَبَّكُمُ الَّذِي خَلَقَكُم مِّن نَّفْسٍ وَاحِدَةٍ وَخَلَقَ مِنْهَا زَوْجَهَا وَبَثَّ مِنْهُمَا رِجَالًا كَثِيرًا وَنِسَاءً ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ الَّذِي تَسَاءَلُونَ بِهِ وَالْأَرْحَامَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلَيْكُمْ رَقِيبًا

“Enyi watu! Mcheni Mola wenu ambaye amekuumbeni kutokana na nafsi moja na akaumba kutoka humo mke wake na akaeneza kutoka hao wawili wanaume na wanawake wengi na mcheni Allaah ambaye Kwaye mnaombana na jamaa zenu. Hakika Allaah daima amekuwa juu yenu ni Mwenye kuchunga.” (04:01)

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَقُولُوا قَوْلًا سَدِيدًا يُصْلِحْ لَكُمْ أَعْمَالَكُمْ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ ۗ وَمَن يُطِعِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ فَازَ فَوْزًا عَظِيمًا

“Enyi walioamini! Mcheni Allaah na semeni kauli ya sawasawa. Atakutengenezeeni matendo yenu na atakusameheeni madhambi yenu; na anayemtii Allaah na Mtume wake, basi kwa hakika amefanikiwa mafaniko makubwa.” (33:70-71)

Amma ba´d:

Hakika maneno ya kweli kabisa ni Kitabu cha Allaah. Uongofu bora ni wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Uovu wa mambo ni yale ya kuzua. Kila kilichozuliwa ni Bid´ah. Kila Bid´ah ni upotevu. Kila upotevu ni Motoni.

Amma baada ya hayo; sidhani kuwa naweza kuwasilisha katika hafla hii tukufu – na khaswa ukizingatia ya kwamba ndani yake kuna wanachuoni watukufu na maustadhi waheshimiwa – kitu katika elimu ambacho hakikuwahi kugusiwa. Inatosheleza kwangu kwa maneno yangu mafupi haya niwe ni mwenye kukumbusha na mwenye kufuata maneno ya Allaah (Tabaarak wa Ta´ala):

وَذَكِّرْ فَإِنَّ الذِّكْرَىٰ تَنفَعُ الْمُؤْمِنِينَ

“Kumbusha, kwani hakika ukumbusho unawafaa waumini.” (51:55)

Mada yangu katika usiku huu uliobarikiwa wa Ramadhaan naonelea iwe katika kubainisha kitu katika fadhila zake, hekima zake na ubora wa kusimama nyusiku zake na mfano wa hayo kama ilivyozoeleka kwa wale wenye kutoa mawaidha na maelekezo katika mambo yatayowafaa wafungaji na yawapelekee katika kheri na baraka. Nimechagua mazungumzo yangu yawe katika utafiti ambao ni muhimu sana. Ni msingi miongoni mwa misingi ya Shari´ah; kubainisha umuhimu wa Sunnah katika Shari´ah ya Uislamu.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Manzilat-us-Sunnah fiyl-Islaam, uk. 4-6
  • Imechapishwa: 10/02/2017