Ni neno linalosemwa na waislamu katika adhaana zao, pindi wanapokimu swalah, khutbah zao na katika mazungumzo yao. Ni neno ambalo ardhi na mbingu zimesimama kwa ajili yake. Ni neno ambalo viumbe wote wameumbwa kwa ajili yake. Ni neno ambalo Mitume wametumwa, Vitabu vimeteremshwa na kukawekwa Shari´ah kwa ajili yake. Kwa ajili ya neno hili ndio kukawekwa mizani, madaftari na kukaandaliwa Pepo na Moto. Kwa ajili ya neno hili ndio maana viumbe wamegawanyika kati ya waumini na makafiri. Kwa hiyo ndio chanzo cha uumbaji, amri, thawabu na adhabu. Qiblah kimetengwa na Uislamu umeasisiwa juu yake. Kwa ajili ya neno hili ndio kukawekwa Jihaad. Ndio haki ya Allaah juu ya viumbe wote. Ndio neno la Uislamu na vilevile ndio ufunguo wa Pepo. Neno hilo wataulizwa viumbe wa mwanzo na wa mwisho. Mja hatopiga hatua mbele ya Allaah isipokuwa ataulizwa maswali mawili:

1 – Ulikuwa unaabudia nini?

2 – Uliwajibu nini Mitume?

Jibu ya swali la kwanza ni kwa kuhakikisha shahaadah kwa kuitambua, kuikubali na kuitendea kazi.

Jibu ya swali la pili ni kwa kuhakikisha ´Muhammad ni Mtume wa Allaah` kwa kuijua, kunyenyekea kwayo na kumtii.

Neno hili ndilo lenye kutenganisha kati ya ukafiri na Uislamu, neno la uchaji, kishikilio madhubuti na vilevile ndio neno ambalo Ibraahiym:

وَجَعَلَهَا كَلِمَةً بَاقِيَةً فِي عَقِبِهِ لَعَلَّهُمْ يَرْجِعُونَ

“Akalifanya ni neno lenye kubakia katika kizazi chake ili wapate kurejea.” (43:28)

Ndio neno ambalo Allaah amejishuhudia juu Yake Mwenyewe, Malaika na wanazuoni pia wakamshuhudilia. Amesema (Ta´ala):

شَهِدَ اللَّـهُ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ وَالْمَلَائِكَةُ وَأُولُو الْعِلْمِ قَائِمًا بِالْقِسْطِ ۚ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ

“Allaah ameshuhudia kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Yeye, Malaika na wenye elimu [pia wameshuhudia], ni Mwenye kusimamisha kwa uadilifu. Hapana mungu wa haki isipokuwa Yeye, Mwenye nguvu kabisa asiyeshindika, Mwenye hekima.” (03:18)

Ndio neno la ikhlaasw, shahaadah ya kweli, wito wa kweli na lililojitenga mbali na shirki. Viumbe wameumbwa kwa ajili ya neno hili. Amesema (Ta´ala):

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ

“Sikuumba majini na watu isipokuwa waniabudu.” (51:56)

Mitume wametumwa na Vitabu vikateremshwa kwa ajili ya neno hili. Amesema (Ta´ala):

وَمَا أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ مِن رَّسُولٍ إِلَّا نُوحِي إِلَيْهِ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنَا فَاعْبُدُونِ

“Hatukutuma kabla yako Mtume yeyote isipokuwa Tulimfunulia Wahy ya kwamba: “Hakika hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Mimi; hivyo basi niabuduni.” (21:25)

يُنَزِّلُ الْمَلَائِكَةَ بِالرُّوحِ مِنْ أَمْرِهِ عَلَىٰ مَن يَشَاءُ مِنْ عِبَادِهِ أَنْ أَنذِرُوا أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنَا فَاتَّقُونِ

“Anateremsha Malaika na Roho kwa amri Yake kwa Anayemtaka miongoni mwa waja Wake kwamba waonye kuwa hapana mungu wa haki isipokuwa Mimi; hivyo basi nicheni.” (16:02)

Ibn ´Uyaynah amesema:

“Hakuna neema kubwa Allaah amemneemesha mja kama kumfunza shahaadah na kwamba shahaadah ni ya watu wa Peponi kama ambavyo maji ya baridi ni ya watu wa duniani.”[1]

Mwenye kulitamka inasamilika mali na damu yake. Mwenye kukataa kulitamka mali na damu yake ni vyenye kuchukiliwa. Imepokelewa katika “as-Swahiyh” ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atayesema ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah` na akakufuru vile vyenye kuabudiwa badala ya Allaah, imeharamika mali na damu yake na hesabu yake iko kwa Allaah.”[2]

Ndio kitu cha kwanza wanachotakwa makafiri pindi wanapolinganiwa katika Uislamu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pindi alipomtuma Mu´aadh kwenda Yemen alimwambia:

“Hakika wewe unawaendea watu katika Ahl-ul-Kitaab. Hivyo basi, iwe jambo la kwanza utalowalingania kwalo ni kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah… “[3]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Kwa haya itapata kutambulika ina nafasi gani katika Uislamu, umuhimu wake katika maisha na kwamba ndio jambo la kwanza la wajibu kwa mja. Kwa kuwa ndio msingi uliyojengwa juu yake matendo yote.

[1] Kalimat-ul-Ikhlaasw, uk. 52-53 ya Ibn Rajab.

[2] Muslim (23) na Ahmad (06/394).

[3] al-Bukhaariy (1389), Muslim (19) na at-Tirmidhiy (265).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnaja.com
  • Marejeo: Ma´naa laa ilaaha illa Allaah, uk. 9-12
  • Imechapishwa: 23/09/2023