02. Msingi wa kwanza: kumtakasia dini Allaah

Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimhu Allaah) amesema:

Msingi wa kwanza:

Kumtakasia dini Allaah (Ta´ala), hali ya kuwa pekee hana mshirika

MAELEZO

Msingi wa kwanza katika misingi hii sita ni kumtakasia dini Allaah, hali ya kuwa pekee hana mshirika. Huu ndio msingi wa misingi na pia ndio msingi wa dini. Msingi huu ndio sababu ya magomvi kati ya Mitume na watu wao. Mitume wanachotaka ni kusahihisha msingi huu ambao ndio sababu ya Allaah kuwaumba viumbe kwa ajili yake na akafungamanisha furaha na kufaulu kwao kwa msingi huu.

Muhimu sio kwa mtu kufunga, kuswali na kufanya ´ibaadah chungumzima. Lililo muhimu ni kuwa na kumtakasia nia Allaah. Matendo machache yaliyofanywa kwa ajili ya Allaah pekee ni bora kuliko matendo mengi ambayo hayakufanywa kwa ajili ya Allaah. Lau mtu ataswali usiku mzima na mchana, akatoa mapesa mengi na kufanya matendo mengi pasi na kumtakasia nia Allah, hakuna faida yoyote katika matendo yake. Kumtakasia nia Allaah ni jambo la lazima.

Kumtakasia nia Allaah (Ikhlaasw) maana yake ni kuacha shirki na badala yake kumpwekesha Allaah (Jalla wa ´Alaa) kwa ´ibaadah. Hakuna yeyote anayestahiki ´ibaadah, pasi na kujali ukamilifu na ubora ataokuwa nao, isipokuwa Allaah (Jalla wa ´Alaa). Haijalishi kitu ni mamoja awe ni Malaika walio karibu, Manabii na Mitume wala mawalii na waja wema. Huu ndio msingi. Msingi huu hauhakikishwi isipokuwa kwa mtu kuacha shirki. Yule mwenye kuchanganya kati ya kumuabudu Allaah na kushirikisha wengine, huyu matendo yake ni yenye kuharibika. Kuhusiana na yule mwenye kumtakasia matendo yake Allaah (´Azza wa Jall), huyu ndiye mwenye furaha na kufaulu ijapo matendo yake yatakuwa machache. Matendo machache yaliyoambatana na kumtakasia nia Allaah, ndani yake mna kheri na uokozi. Hadiyth ya kadi ni yenye kutambulika:

“Kuna mtu atafufuliwa siku ya Qiyaamah ili kufanyiwa hesabu na Allaah (Tabaarak wa Ta´ala). Matendo yake maovu yawekwe kwenye sahani la mzani mbele yake, madhambi mengi sawa na upeo macho yanaweza kufika. Kwenye sahani lingine la mzani kuwekwe kadi ilio na ´laa ilaaha illa Allaah` ambapo mtu huyu aliisema kwa utakasifu wa nia, yakini na imani kutoka kwa moyoni mwake. Neno hili liwe na nguvu juu ya kadi zote na lishinde kadi zote.”

Huku ndio kumtakasia nia Allaah. Hakuitamka tu kimatamshi. Bali aliisema huku akijua maana yake na akiamini yale yenye kujulishwa nalo. Lakini mtu huyu alikufa kabla ya kuwa na uwezo wa kufanya matendo. Vipi kwa ambaye yuko na matendo mengi ambayo ni mema aliyafanya kwa kutafuta uso wa Allaah (´Azza wa Jall)? Hili linafahamisha kwamba kumtakasia nia Allaah, ijapo utakasifu nia utakuwa ndogo, Allaah anaweza kumwokoa mwenye nayo kwa ajili yake na ikawa ni sababu ya Allaah kumsamehe madhambi na maasi yake yote. Upande mwingine utakasifu nia ukikosekana, basi hakuna faida ya wingi wa matendo.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sittah, uk. 09-10
  • Imechapishwa: 18/05/2021