Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

1- Allaah (Ta´ala) amesema:

مَا أَصَابَ مِن مُّصِيبَةٍ إِلَّا بِإِذْنِ اللَّـهِ ۗ وَمَن يُؤْمِن بِاللَّـهِ يَهْدِ قَلْبَهُ ۚ وَاللَّـهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ

“Hausibu msiba wowote [kukupateni] isipokuwa kwa idhini ya Allaah. Yeyote   anayemuamini Allaah, basi huuongoza moyo wake. – Allaah kwa kila kitu ni mjuzi.”[1]

´Alqamah amesema:

“Huyo ni yule mtu ambaye anapofikwa na msiba anajua kuwa umetoka kwa Allaah, basi akaridhika na akajisalimisha.”

2- Muslim amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mambo mawili kwa watu ni kufuru; kutukaniana nasabu na kuomboleza juu ya maiti.”[2]

3- al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba amesema:

“Si katika sisi yule mwenye kujipiga kwenye mashavu, akachana nguo na akaita kwa mayowe ya kipindi cha kikafiri.”[3]

4- Anas (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah anapomtakia mja Wake kheri, basi humharakishia adhabu duniani, na anapomtakia mja Wake shari, humcheleweshea adhabu ya dhambi yake mpaka siku ya Qiyaamah.”[4]

5- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ukubwa wa malipo ni pamoja na ukubwa wa mitihani. Hakika Allaah (Ta´ala) anapowapenda watu basi huwapa huwajaribu. Yule mwenye kuridhia basi hupata radhi Zake na yule mwenye kuchukia basi hupata hasira Zake.”[5]

Ni nzuri kwa mujibu wa at-Tirmidhiy.

MAELEZO

Mnasaba wa mlango huu na Kitaab-ut-Tawhiyd ni kwamba kuwa na subira juu ya makadirio ya Allaah ni katika mambo yanayoikamilisha Tawhiyd. Kama ambavyo kutokuwa na subira juu ya makadirio ya Allaah ni miongoni mwa mambo yanayoipunguza Tawhiyd. Shaykh ametunga kitabu hichi kilichobarikiwa kwa ajili ya kuibainisha Tawhiyd na yale yenye kuikamilisha na yaliyo kinyume chake na yenye kuidhoofisha.

Mwandishi (Rahimahu Allaah) amesema:

“Katika kumwamini Allaah… “

Miongoni mwa sifa na matawi ya kumwamini Allaah (´Azza wa Jall) ni kule mtu kuwa na subira juu ya makadirio ya Allaah. Kunaingia ndani ya kumwamini Allaah ambako ni moja katika zile nguzo sita za imani. Kwa mujibu wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah imani ni kutamka kwa ulimi, matendo ya viungo na kuamini ndani ya moyo. Inazidi kwa matendo mema na inashuka kwa matendo maovu. Hii ndio imani.

Mwandishi amesema:

“… ni kule kuwa na subira juu ya makadirio ya Allaah.”

Maana ya subira kilugha ni kule kujizuia. Allaah (Ta´ala) amesema kumwambia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

وَاصْبِرْ نَفْسَكَ مَعَ الَّذِينَ يَدْعُونَ رَبَّهُم بِالْغَدَاةِ وَالْعَشِيِّ يُرِيدُونَ وَجْهَهُ ۖ وَلَا تَعْدُ عَيْنَاكَ عَنْهُمْ تُرِيدُ زِينَةَ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا

“Isubirishe nafsi yako pamoja na wale wanaomuomba Mola wao asubuhi kabla jua kucha na jioni, wanataka uso Wake, na wala macho yako yasiwavuke kwa kutaka pambo la uhai wa dunia.”[6]

Bi maana izuie pamoja na watu hawa.

Maana ya subira Kishari´ah ni kuizuia nafsi ili imtii Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) na iache kumuasi.

[1] 64:11

[2] Muslim (67).

[3] al-Bukhaariy (1294) na Muslim (103).

[4] at-Tirmidhiy (2396), al-Haakim (8799) na Abu Ya´laa (4254). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ul-Jaami´” (308).

[5] at-Tirmidhiy (2396) na Ibn Maajah (4031). Nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ul-Jaami´” (2110).

[6] 18:28

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: I´aanat-ul-Mustafiyd bi Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 430
  • Imechapishwa: 13/08/2019