01. Kosa la kwanza katika ´Aqiydah: Kupinga ujuu wa Allaah

Nimefikiwa na khabari kwamba watu wengi wanatumbukia katika makosa mengi yanayohusu ´Aqiydah na katika mambo wanayofikiria kuwa ni Sunnah ilihali ni Bid´ah. Miongoni mwa mambo hayo ni yafuatayo:

1- Kupinga ujuu wa Allaah na kulingana Kwake juu ya ´Arshi Yake. Ni jambo linalotambulika kuwa Allaah (Subhaanah) amebainisha jambo hilo katika Kitabu Chake kitukufu pale aliposema (Subhaanah):

إِنَّ رَبَّكُمُ اللَّـهُ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ

“Hakika Mola wenu ni Allaah ambaye ameumba mbingu na ardhi katika siku sita kisha akalingana juu ya ´Arshi.”[1]

Ametaja jambo hilo katika Aayah saba kutoka katika Kitabu Chake kitukufu. Miongoni mwazo ni Aayah hii.

Isitoshe wakati Maalik (Rahimahu Allaah) alipoulizwa juu ya hilo akasema:

”Kulingana kunatambulika, namna haijulikani, kuamini hilo ni lazima.”

Wako maimamu wengine katika Salaf waliosema maneno haya.

Maana ya ”kulingana kunatambulika” ni kwa upande wa lugha ya kiarabu. Ni kuwa juu. Amesema (Subhaanah):

فَالْحُكْمُ لِلَّـهِ الْعَلِيِّ الْكَبِيرِ

“Basi hukumu ni ya Allaah pekee, Aliye juu kabisa, Mkubwa.”[2]

وَهُوَ الْعَلِيُّ الْعَظِيمُ

“Naye yujuu kabisa, Ametukuka.”[3]

إِلَيْهِ يَصْعَدُ الْكَلِمُ الطَّيِّبُ وَالْعَمَلُ الصَّالِحُ يَرْفَعُهُ

“Kwake linapanda neno zuri na tendo zuri hulitukuza.”[4]

Zipo Aayah nyenginezo nyingi zinazojulisha uwepo juu na kwamba Yeye (Subhaanah) yuko juu ya ´Arshi na juu ya viumbe wengine wote.

Haya ndio maoni ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah katika Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wengineo.

[1] 07:54

[2] 40:12

[3] 02:255

[4] 35:10

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Akhtwaau fiyl-´Aqiydah, uk. 1
  • Imechapishwa: 18/06/2020