01. Kitu cha kwanza ambacho kila Mtume alikuwa akiwalingania watu wake

Himdi zote anastahiki Allaah, Mola wa walimwengu. Swalah na salaam zimwendee Mtume wetu Muhammad ambaye ndiye Mtume wa mwisho na wale wote watakaoshikamana barabara na Sunnah zake na wakapita juu ya mwongozo wake mpaka siku ya Qiyaamah.

Amma ba´d:

´Aqiydah ndio msingi ambao yamesimama juu yake majengo ya nyumati zote. Kufaulu kwa kila Ummah kumefungamana na kusalimika kwa ´Aqiydah na fikira zake. Kwa ajili hiyo ndio maana nyujumbe za Mitume wote (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) zimekuja zikitangaza kurekebisha ´Aqiydah. Kila Mtume kitu cha kwanza alichokuwa akiwaambia watu wake anapowalingania:

اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ

“Enyi watu wangu! Mwabuduni Allaah, kwani hamna mwabudiwa wa haki mwingine asiyekuwa Yeye.”[1]

وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِي كُلِّ أُمَّةٍ رَّسُولًا أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ وَاجْتَنِبُوا الطَّاغُوتَ

”Hakika Tulituma katika kila ummah Mtume kwamba: “Mwabuduni Allaah na jiepusheni na Twaaghuut [waungu batili].”[2]

Hilo ni kwa sababu Allaah (Subhaanah) amewaumba viumbe ili waweze kumuabudu Yeye pekee (Subhaanahu wa Ta´ala). Amesema (Ta´ala):

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ

“Sikuumba majini na watu isipokuwa waniabudu.”[3]

[1] 07:59

[2] 16:36

[3] 51:56

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan Haqiyqat-it-Tawhiyd, uk. 03-04
  • Imechapishwa: 30/07/2018