KITABU CHA TWAHARA

Nia na hukumu zake

1-

عَنْ أمِيرِ المُؤْمِنِينَ أبي حَفْصِ ” عُمَرَ بْنِ الخَطَاب ” رَضيَ الله عَنْهُ قَال: سَمِعت رسُولَ الله صَلّى الله عَلَيْهِ وَسَلَّم يَقُول
إنَّمَا الأعْمَالُ بَالْنيَاتِ، وَإنَّمَا لِكل امرئ مَا نَوَى، فمَنْ كَانَتْ هِجْرَتهُ إلَى الله وَرَسُولِهِ فَهِجْرَتهُ إلَى الله وَرَسُولِهِ، وَمَنْ كَانَتْ هِجْرتُهُ لِدُنيا يُصيبُهَا، أو امْرَأة يَنْكِحُهَا فَهِجْرَتُه إلَى مَا هَاجَرَ إليهِ

Kiongozi wa waumini Abu Hafswah ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) amesema: “Nimemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Hakika kila kitendo kinategemea na nia na kila mmoja atalipwa kwa kile alichonuia. Yule ambaye kuhajiri kwake kutakuwa kwa ajili ya Allaah na Mtume wake, basi kuhajiri kwake kutakuwa kwa ajili ya Allaah na Mtume. Yule ambaye kuhajiri kwake kutakuwa kwa ajili ya dunia au mwanamke anayetaka kumuoa, basi kuhajiri kwake kutakuwa kwa lile aliloliendea.”

Hadiyth hii ni kubwa na ni kanuni tukufu miongoni mwa kanuni za Kiislamu. Ni kipimo (Qiyaas) sahihi kinachotumiwa kuyapima matendo kwa njia ima ya kukubaliwa au kukataliwa, wingi wa thawabu au uchache wake.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anaelezea ya kwamba matendo yanazungukia katika nia. Nia ikiwa njema na matendo yakafanywa kwa ajili ya Allaah pekee, basi matendo ni yenye kukubaliwa. Matendo yakiwa yamefanywa kwa malengo mengine, ni yenye kukataliwa. Hakika Allaah (Ta´ala) amejitosheleza kabisa kutokamana na shirki.

Nia inatofautisha ´ibaadah na mambo ya kawaida. Kwa mfano yule mwenye kuoga na huku anakusudia kuondosha josho la najaba, hii inakuwa ´ibaadah. Mwingine anaoga na huku anakusudia kujisafisha au kupata baridi kidogo, inakuwa jambo la kawaida.

FAIDA KATIKA HADIYTH

1- Matendo yanazungukia nia, sawa kusihi au kuharibika kwake, kutimia kwake au kupungua kwake, utiifu au maasi. Yule ambaye kwa kitendo chake atakusudia kujionyesha, basi anapata dhambi. Yule ambaye kwa mfano kwa kupigana Jihaad atakusudia kulinyanyua neno la Allaah liwe juu, thawabu zake zinakuwa kamilifu. Atakayekusudia kwa Jihaad hiyo kulinyanyua neno la Allaah pamoja na kupata ngawira, thawabu zake zinapungua. Atakayekusudia kupata ngawira peke yake, hakupata dhambi lakini hata hivyo hapati thawabu kama za Mujaahid.

2- Hakika nia ni sharti ya msingi katika matendo. Lakini pasi na kuvuka mipaka ya kuihudhurisha na kusema asiyefanya hivo ´ibaadah yake inaharibika. Hakika kule kutaka kufanya kitendo ndio kutia nia. Huna makalifisho ya kuihudhurisha na kuihakikisha.

3-  Nia mahala pake ni moyoni. Kutamka nia ni Bid´ah.

4- Uwajibu wa kutahadhari kutokamana na kujionyesha, kutaka kusikika na mtu akafanya kitendo kwa ajili ya kutaka dunia, kwani mambo hayo yanaiharibu ´ibaadah.

5- Uwajibu wa kutilia mkazo matendo ya moyo na kuchungana nayo.

6- Mtu kuhama kutoka mji wa kikafiri na kuhamia mji wa Kiislamu ni katika ´ibaadah zilizo bora kabisa iwapo mtu atakusudia Uso wa Allaah (Ta´ala).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdullaah bin ´Abdir-Rahmaan al-Bassaam
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Taysiyr-ul-´Allaam Sharh ´Umdat-il-Ahkaam (01/15-17)
  • Imechapishwa: 21/08/2017