01. Ibn Laadin – Mujaahid Au Muharibifu?


Swali: Watu wana maoni tofauti juu ya kiongozi wa al-Qaa´idah Usaamah bin Laadin. Kuna ambao wanaonelea kuwa ni mtu mwenye kuinusuru Dini ya Allaah na kuongoza Jihaad kwa sababu ameshambulia nchi nyingi za manaswara kwa fikira na maelekezo yake ambayo yamesababisha khasara kubwa. Ukiongezea juu ya hilo ana wanaharakati wa Jihaad wengine ambao ni miji michache mno imesalimika nao.

Wengine wanaonelea kuwa Usaamah bin Laadin ambaye Allaah Amemtunukia mali kutoka Saudi Arabia kabla ya kuanza kueneza ufisadi katika ardhi alibadilika kwa mali na fikira zake zilizopinda na kwamba anaeneza ufisadi ulimwenguni kote. Anaomba msaada wa kifedha na anacheza kimaneno na watu wenye akili pungufu na imani dhaifu kupitia hutuba zilizopinda zinazorushwa kwenye vyombo vya khabari kutoka kwenye majibali ya Afghanistan na maeneo ya jirani yake.

Ni kundi lepi katika haya mawili lililo na haki katika hili kuhusiana na mtu huyu ambaye ameusababishia Uislamu na Waislamu shari yenye kuendelea na uharibifu ulio mkubwa? Ninataraji jibu litaandikwa. Allaah Akujaze kheri na Akufanye uielewe Dini.

Jibu: Unatakiwa kutambua ya kwamba wale wenye kusema kuwa Usaamah bin Laadin anainusuru Dini, analingania katika haki na matapo mengine ima ni wajinga walioipa haki mgongo. Hawana udhuru wowote wa kuipa haki mgongo. Au ni watu wa jarima walio na ujuzi ni nani aliye na haki na kukosea lakini wanaeneza ufisadi katika ardhi na chuki imewajaa dhidi ya watawala wa Kiislamu na wanachuoni ambao Allaah Amewatunukia uelewa katika Dini. Dhambi ya watu hawa ni mbaya zaidi. Adhabu yao mbele ya Allaah ni kubwa sana kwa kwenda kinyume na haki, kueneza ufisadi katika ardhi na kuua watu pasina haki.

Kujengea juu ya hili wafuasi wa Usaamah bin Laadin hawana dalili juu ya kwamba Usaamah bin Laadin ni Mujaahid mwenye kuinusuru Dini. Hawana dalili ya hilo kutoka katika Shari´ah, akili, desturi yenye kuingia akilini au nidhamu yenye kukubalika. Wanachoweza tu ni kuleta ubishi wa batili na kuwatia wajinga na watu wenye imani dhaifu mchanga wa machoni. Kwa njia hiyo wamepotea na kuwapoteza wengine wengi kutoka kwenye njia iliyonyooka.

Ikiwa umeshangazwa basi ushangae zaidi wanasema ya kwamba Ibn Laadin amepambana kwa maisha yake na mali yake kwa ajili ya Uislamu na Jihaad. Uhakika wa mambo ni kwamba yeye na wafuasi wake wanaeneza ufisadi katika ardhi kwa kwenda kinyume na maamrisho ya Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na njia ya waumini. Wamechafua nyayo za Uislamu. Wamewatisha watu na Uislamu. Uislamu hauna lolote kuhusiana na matendo yao machafu. Uislamu ni Dini ya uadilifu na rehema na yenye kutimiza ahadi. Sio Dini ya hadaa, vitimbi na utovu wa adabu.

  • Mhusika: ´Allaamah Zayd bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Waqafaat wa Ma´aalim, uk. 5-7
  • Imechapishwa: 29/11/2014