Hili ni suala kubwa ambalo wanachuoni katika zama zote wametofautiana kwalo. Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Mwenye kuacha swalah ni kafiri. Ukafiri wake ni mkubwa wenye kumtoa katika Uislamu. Anatakiwa kuuawa endapo hatotubia na kuanza kuswali.”

Abu Haniyfah, Maalik na ash-Shaafi´iy wamesema:

“Ni mtenda dhambi kubwa lakini hakufuru.”

Baada ya hapo wakatofautiana. Maalik na ash-Shaafi´iy wamesema:

“Anatakiwa kuuawa kama mtenda dhambi.”

Abu Haniyfah akasema:

“Anatakiwa kuaziriwa na wala asiuawe.”

Midhali masuala haya yana tofauti basi ni wajibu kuyarudisha katika Kitabu cha Allaah na Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَا اخْتَلَفْتُمْ فِيهِ مِن شَيْءٍ فَحُكْمُهُ إِلَى اللَّـهِ

“Na katika lolote lile mlilokhitilafiana, basi hukumu yake ni kwa Allaah.”[1]

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنكُمْ ۖ فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا

“Enyi mlioamini! Mtiini Allaah na mtiini Mtume na wenye madaraka katika nyinyi. Mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Allaah na Mtume mkiwa mnamwamini Allaah na siku ya Mwisho. Hili ni bora na matokeo mazuri kabisa.”[2]

Maoni ya yeyote hayawi ni hoja juu ya maoni ya mwingine kwa sababu kila mmoja anaonelea kuwa maoni yake ndio ya sawa. Hakuna maoni ya ambaye yana haki zaidi ya kukubaliwa kuliko ya mwingine. Kwa ajili hiyo ni wajibu kulirejesha suala hili katika hukumu yenye kuhukumu, nayo ni Kitabu cha Allaah (Ta´ala) na Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Endapo tutalirudisha suala hili katika Qur-aan na Sunnah basi tunapata kuona kuwa vyote viwili vinathibitisha kuwa asiyeswali ni kafiri ambaye ukafiri wake unamtoa katika Uislamu.

[1] 42:10

[2] 04:59

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Hukm Taarik-is-Swalaah, uk. 3
  • Imechapishwa: 22/10/2016