01. Hakuna dalili yoyote sahihi kuwa Israa´ na Mi´raaj ilikuwa usiku gani

Himdi zote anastahiki Allaah pekee. Swalah na amani zimwendee Mtume wa Allaah, kizazi chake na Maswahabah zake.

Amma ba´d:

Ni jambo lisilokuwa na shaka yoyote kuwa Israa´ na Mi´raaj ni katika alama kubwa za Allaah zenye kutolea dalili kufahamisha ukweli wa Mtume Wake Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ukubwa wa manzilah yake mbele ya Allaah (´Azza wa Jall). Vilevile kuna dalili juu ya uwezo wa Allaah na kufahamisha kuwa yuko juu ya viumbe Wake wote (Subhaanah). Allaah (Ta´ala) amesema:

سُبْحَانَ الَّذِي أَسْرَىٰ بِعَبْدِهِ لَيْلًا مِّنَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ إِلَى الْمَسْجِدِ الْأَقْصَى الَّذِي بَارَكْنَا حَوْلَهُ لِنُرِيَهُ مِنْ آيَاتِنَا ۚ إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Utakasifu ni wa Ambaye amemsafirisha mja Wake usiku kutoka al-Masjid al-Haraam mpaka al-Masjid al-Aqswaa ambao Tumevibariki vilivyoko pembezoni mwake [amechukuliwa] ili Tumuonyeshe baadhi ya alama Zetu. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia yote daima, Mwenye kuona yote daima.”[1]

Imepokelewa kwa njia mbalimbali kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba alipandishwa mbinguni na akafunguliwa milango yake mpaka akapita mbingu ya saba. Mola Wake akamzungumzisha kwa yale aliyoyataka na akafaradhisha juu yake swalah tano. Mwanzoni (Subhaanah) alikuwa amemfaradhishia swalah khamsini. Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuacha kuwa ni mwenye kurejea Kwake na kumuomba uwepesishiwe mpaka akamfanyia zikawa tano. Ni faradhi tano lakini hata hivyo inapokuja katika thawabu ni khamsini; kwa sababu tendo jema moja linalipwa mara kumi – himdi na shukurani njema zote anastahiki Allaah.

Hakukuja katika Hadiyth Swahiyh yoyote yenye kusema kuwa Israa´ na Mi´raaj ilikuwa ni usiku fulani. Kila kilichokuja kulenga usiku maalum hakikuthibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa mujibu wa wanachuoni wa Hadiyth. Allaah ni mwingi wa hekima kwa kuwasawazisha nayo watu. Lau hata kungelithibiti kuwa ni usiku maalum basi isingelijuzu kwa waislamu kukhusisha ndani yake kwa kufanya kitu chochote kile katika ´ibaadah na isingelijuzu kuusherehekea kwa kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake hawakusherehekea na wala hawakufanya kitu maalum siku hiyo. Ikiwa kusherehekea ni kitu kimechowekwa katika Shari´ah basi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) angewabainishia Ummah kwa maneno au vitendo. Lau kungelipitika kitu katika hayo kingejulikana na kuwa wazi na hivyo Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) wangetunukulia. Kwani wametunukulia kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yale yote ambayo Ummah unayahitajia na hawakupuuzia chochote kinachohusiana na dini.

[1] 17:01

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tahdhiyr minal-Bid´ah, uk. 15-17
  • Imechapishwa: 19/01/2022