01. Hadiyth “Wakati nilipokuwa nimelala walinijia watu wawili… “

1005- Abu Umaahah al-Baahiliy (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Wakati nilipokuwa nimelala walinijia watu wawili wakanishika mkono wangu. Wakanipeleka kwenye mlima usiyokuwa sawa na wakasema: “Panda.” Nikasema: “Siwezi.” Wakasema: “Hakika sisi tutakurahisishia.” Nikapanda. Nilipofika katikati ya mlima ghafla nikasikia kelele kali. Nikasema: “Ni zipi kelele hizi?” Wakasema: “Hizi ni kelele za watu wa Motoni.” Kisha akanipeleka na nikawafikia watu wengine walioning´inizwa kwenye visigino vyao. Sehemu za pembeni za midomo yao zimekatikakatika na damu inatiririka. Nikasema: “Ni watu gani hawa?” Wakasema: “Ni wale wanaofuturu kabla ya kumalizika kwa swawm zao[1].”[2]

Ameipokea Ibn Khuzaymah na Ibn Hibbaan katika “as-Swahiyh” zao.

[1] Bi maana kabla ya jua kuzama na si kabla ya adhaana, kama wanavofikiria baadhi ya wajinga. Kwa ajili hiyo utawaona wanawakemea wale wanaokata swawm zao pale tu wakati jua linazama kwa ajili ya kufuata Sunnah na kwenda kinyume na Shiy´ah. Wanalazimisha kuchelewesha funga mpaka wakati wa adhaana ambayo wakati mwingine inaweza kuchelewa takriban dakika kumi katika baadhi ya miji ya Kiislamu. Kwa sababu wanaadhini kwa kutegemea jadwali ya unajimu na sio kwa kutazama kwa macho. Masaa yanatofautiana kutoka katika wilaya moja kwenda kwa wilaya nyingine, mji mmoja kwenda katika mji mwingine bali mkoa mmoja kwenda katika mkoa mwingine katika nchi hiyohiyo moja. Katika baadhi ya miji nimeshuhudia mwenyewe kusikia adhaana licha ya kuwa jua bado lachomoza.

[2] Swahiyh.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Adhwiym bin ´Abdil-Qawiy al-Mundhiriy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swahiyh-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb (1/588)
  • Imechapishwa: 22/04/2020
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy