134- Ubayy bin Ka´b (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Muusa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisimama akitoa Khutbah kwa wana wa israaiyl ambapo akaulizwa: “Ni mtu gani mjuzi zaidi?” Akajibu: “Mimi ndiye mjuzi zaidi.” Allaah akamlaumu kwa vile hakuirudisha elimu Kwake na akamteremshia Wahy: “Nina mja wangu ambaye yuko pale ambapo yanapokutana maji ya bahari mbili ni mjuzi zaidi kuliko wewe.” Akasema: “Ee Mola wangu! Ni vipi nitamfikia.”Akaambiwa: “Mchukue samaki kwenye kikapu. Pale utapomkosa basi anapatikana hapo…

Wakaanza kutembea kando na bahari hali ya kuwa hawana safina. Walipokuwa wanaendelea na safari yao wakaipitia safina ambapo wakawaomba wawape lifti. Wakamtambua Khadhwir na akawaacha waingie ndani bila malipo. Akaja ndege na akatua kwenye ukingo wa ile safina na akadonoa mara moja au mara mbili ndani ya bahari ile. Khadhwiyr akasema: “Ee Muusa! Elimu yangu mimi na wewe ukilinganisha na elimu ya Allaah haikupunguza chochote isipokuwa kama mfano wa ndege huyu alivodonoa ndani ya bahari hii.”

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Wakati Muusa alipokuwa anatembea kati ya wana wa israaiyl alikuja bwana mmoja na kumwambia: “Unamjua yeyote ambaye ni mjuzi zaidi kukushinda?” Muusa akajibu: “Hapana.” Ndipo Allaah akamteremshia Wahy Muusa akimwambia: “Ndio, mja Wetu Khadhwiyr.” Ndipo Muusa akamuuliza njia ya kumfikia.”[1]

Ameipokea al-Bukhaariy, Muslim na wengineo.

[1] Swahiyh.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Adhwiym bin ´Abdil-Qawiy al-Mundhiriy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swahiyh-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb (1/165-166)
  • Imechapishwa: 06/05/2020
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy