01. Hadiyth “Msiitangulizie Ramadhaan kwa kufunga siku siku au mbili… “


Hadiyth ya kwanza:

1- Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Msiitangulizie Ramadhaan kwa kufunga siku moja au mbili. Isipokuwa mtu ambaye alikuwa akifunga swawm. Basi aiendeleze.”

Maana ya kijumla:

Shari´ah yenye hekima inataka kutofautisha kati ya ´ibaadah na desturi na inataka kutofautisha kati ya zile ´ibaadah ambazo ni za faradhi na ´ibaadah ambazo zimependekezwa ili kupatikane tofauti kati ya hayo mawili. Kwa ajili hiyo ndio maana imekataza kuitangulizia Ramadhaan kwa kufunga siku moja, mbili au mfano wa hivo ili mtu awe ni mwenye kula na awe tayari kufunga mwezi wa Ramadhaan. Isipokuwa yule ambaye ana mazowea ya kufunga siku ya alkhamisi, jumatatu, kulipa ambako hakujaaliwa wakati mwingine au nadhiri ya lazima, basi afunge. Kwa sababu hayo yamefungamana na sababu. Tofauti na sunnah isiyofungamana. Dogo liwezalo kusemwa ni kwamba imechukizwa.

Faida zinazochukuliwa kutoka katika Hadiyth:

1- Imekatazwa kuitangulizia Ramadhaan kwa kufunga siku moja au mbili.

2- Anapata ruhusa yule ambaye kabla ya Ramadhaan alikuwa na mazowea ya kufunga kama siku ya alkhamisi na jumatatu.

3- Hekima ya hilo – na Allaah ndiye mjuzi zaidi – ni kutofautisha ´ibaadah ambazo ni za faradhi na ´ibaadah ambazo zimependekezwa. Jengine ni ili mtu awe tayari kufunga Ramadhaan kwa uchangamfu na shauku.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdullaah bin ´Abdir-Rahmaan al-Bassaam
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Taysiyr-ul-´Allaam Sharh ´Umdat-il-Ahkaam, uk. (01/313-314)
  • Imechapishwa: 13/05/2018