01. Hadiyth “Matendo yote ya mwanadamu ni yake, isipokuwa swawm… “


978- Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah (´Azza wa Jall) amesema: “Matendo yote ya mwanadamu ni yake[1], isipokuwa swawm. Hiyo ni Yangu mimi na mimi Ndiye nitailipa. Swawm ni kinga[2]. Itapokuwa ni siku ya funga ya mmoja wenu, basi asizungumze maneno machafu wala asipige kelele. Mtu akimtukana au akamgombeza, basi amwambie: “Mimi nimefunga. Mimi nimefunga[3].” Ninaapa kwa Yule ambaye nafsi ya Muhammad iko mikononi Mwake kwamba ile harufu ya mfungaji ni nzuri zaidi mbele ya Allaah kuliko harufu ya miski. Mfungaji ana furaha mbili anazofurahi: anapokata swawm anafurahi kwa futari yake na atapokutana na Mola wake atafurahi kwa funga yake[4].”[5]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim. Tamko ni la al-Bukhaariy. Katika upokezi wa al-Bukhaariy imekuja pia:

“Anaacha chakula chake, kinywaji chake na matamanio yake kwa ajili Yangu. Hivyo swawm ni Yangu mimi. Mimi Ndiye nitailipa. Tendo jema moja linalipwa kwa kumi mfano wake.”

Katika upokezi wa Muslim imekuja:

“Kila kitendo cha mwanadamu kinalipwa maradufu tendo jema moja mara kumi mfano wake mpaka mara mia saba. Allaah (Ta´ala) amesema: “Isipokuwa swawm. Hiyo ni Yangu mimi na mimi Ndiye nitailipa. Anaacha matamanio yake na chakula chake kwa ajili Yangu. Mfungaji ana furaha mbili: furaha ya kwanza ni pale anapokata swawm na furaha nyingine ni pale atapokutana na Mola wake. Ile harufu ya mfungaji ni nzuri zaidi kuliko harufu ya miski.”

Katika upokezi mwingine ambao amepokea yeye na Ibn Khuzaymah imekuja:

“… na pindi atapokutana na Allaah (´Azza wa Jall) atayemlipa atafurahi.”

Ameipokea Maalik, Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na an-Nasaa´iy ikiwa na maana kama hii na matamko tofauti. at-Tirmidhiy amepokea kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mola wenu anasema: “Kila tendo jema moja linalipwa mara kumi mfano wake mpaka mara mia saba. Swawm ni Yangu mimi. Mimi Ndiye nitailipa. Swawm ni kinga dhidi ya Moto. Ile harufu ya mdomoni ya mfungaji ni nzuri zaidi mbele ya Allaah kuliko harufu ya miski. Endapo atakuwepo mjinga mmoja ambaye akamfanyia ujinga mmoja wenu ilihali amefunga basi aseme: “Mimi nimefunga.”[6]

Ibn Khuzaymah amepokea kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah amesema: “Matendo yote ya mwanadamu ni yake, isipokuwa swawm. Hiyo ni Yangu mimi na mimi Ndiye nitailipa. Swawm ni kinga. Ninaapa kwa Yule ambaye nafsi ya Muhammad iko mikononi Mwake kwamba ile harufu ya mdomoni ya mfungaji ni nzuri zaidi mbele ya Allaah siku ya Qiyaamah kuliko harufu ya miski. Mfungaji ana furaha mbili: anapokata swawm anafurahi kwa futari yake na atapokutana na Mola wake atafurahi kwa funga yake.”

Katika upokezi wake mwingine imekuja:

“Amesema: “Matendo yote ya mwanadamu ni yake. Tendo jema moja linalipwa mara kumi mfano wake mpaka mara mia saba.” Allaah amesema: “Isipokuwa swawm. Hiyo ni Yangu mimi na mimi Ndiye nitailipa. Anaacha chakula chake kwa ajili Yangu. Anaacha kinywaji chake kwa ajili Yangu. Anaacha ladha yake kwa ajili Yangu. Anamwacha mke wake kwa ajili Yangu. Ile harufu ya mfungaji ni nzuri zaidi mbele ya Allaah kuliko harufu ya miski. Mfungaji ana furaha mbili: furaha pale anapokata swawm na furaha nyingine ni pale atapokutana na Mola wake.”[7]

Hadiyth ya al-Haarith al-Ash´ariy tayari imekwishatangulia:

“Na nakuamrisheni kufunga. Mfano wa hilo ni kama mtu ambaye amebeba mfuko wa miski na yuko kati ya kundi la watu; kila mmoja anataka kunusa harufu yake. Harufu ya mfungaji ni nzuri zaidi mbele ya Allaah kuliko harufu ya miski.”

at-Tirmidhiy amepokea na akasahihisha maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Harufu ya mfungaji ni nzuri zaidi mbele ya Allaah kuliko harufu ya miski.”

[1] Bi maana yana thawabu maalum, isipokuwa swawm. Swawm inalipwa pasi na hesabu. Kitu kinachotilia nguvu maana hii ni upokezi wa Muslim unaokuja ukiwa na tamko lisemalo: “Kila kitendo cha mwanadamu kinalipwa maradufu tendo jema moja mara kumi mfano wake mpaka mara mia saba. Allaah (Ta´ala) amesema: “Isipokuwa swawm.”

[2] Kwa sababu inamlinda kutokamana na matamanio. Kwani Moto umezungukwa na matamanio, kama ilivyokuja katika Hadiyth Swahiyh:

“Pepo imezungukwa na mambo yenye kuchukiza na Moto umezungukwa na matamanio.”

Ibn-ul-Athiyr amesema:

“Ni kinga kwa sababu inamkinga mwenye nayo kutokamana matamanio yenye kumuudhi.” (an-Nihaayah)

[3] Inawezekana maana yake ni kwamba aseme hivo kwa sauti ili aweze kusikiwa na mara nyingi aweze kukomeka. Inawezekana maana yake ni kwamba aseme hivo kimyakimya ili asiingie katika magomvi. Maoni ya kwanza ndio yenye nguvu zaidi. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

“Maoni sahihi ni kwamba aseme hivo kwa sauti, kama inavyofahamisha Hadiyth. Maneno yasiyofungamana hayawi isipokuwa kwa kutamka.”

[4] Kutokana na vile atavyomlipa.

tika upokezi wa Ahmad imekuja:

“Atapokutana na Mola wake na kumlipa atafurahi.” (Ahmad (2/232))

Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh kwa masharti ya Muslim.

[5] Swahiyh.

[6] Swahiyh kupitia zengine.

[7] Swahiyh.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Adhwiym bin ´Abdil-Qawiy al-Mundhiriy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swahiyh-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb (1/574-577)
  • Imechapishwa: 27/05/2018
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy