Hadiyth “Atakayesimama Ramadhaan kwa imani na kwa matarajio… “

581- Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atakayesimama Ramadhaan kwa imani na kwa matarajio, basi atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia.”

Kumeafikiana kwayo[1].

Faida zinazochumwa kutoka katika Hadiyth:

1- Maana ya “Atakayesimama Ramadhaan” maana yake ni kuhuisha nyusiku zake kwa kufanya ´ibaaah na kuswali. Ndani yake kuna kuwekwa katika Shari´ah swalah ya usiku katika Ramadhaan. Kumethibiti swalah hiyo kuswaliwa kwa mkusanyiko msikitini kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kisha wakaafikiana kwayo Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) katika uongozi wa ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh). Kisha ikatendewa kazi na waislamu wote baada ya hapo ambapo wakaswali swalah ya tarawiyh.

2- Malipo ya kusimama katika mwezi wa Ramadhaan na kusamehewa madhambi. Lakini imekwishatangulia ya kwamba inahusiana na kusamehewa madhambi madogo yanayofungamana na haki ya Allaah (Ta´ala). Dhambi – الذنب – inapotajwa pasi na kufungamanishwa inajumuisha madhambi makubwa na madogo. Lakini Imaam al-Haramayn amesema kwa kukata kabisa ya kwamba inahusiana na madhambi madogo. al-Qaadhwiy ´Iyaadhw akayanasibisha hayo kwa Ahl-us-Sunnah. an-Nawawiy amesema:

“Yasipopatikana madhambi madogo basi kuna matarajio yakapunguzwa madhambi makubwa.”

3- Kukubaliwa kwa swalah ya usiku na kupelekea mtu kusamehewa madhambi yake kwayo kumeshurutishwa mambo mawili:

La kwanza: Kilichompelekea mwenye kusimama kufanya hivo iwe ni imani na kusadikisha thawabu kutoka kwa Allaah (Ta´ala).

La pili: Kufanya kitendo hicho kwa ajili ya Allaah pekee. Kitendo kikikosa masharti haya mawili ambayo ni muhimu na kikaingiwa ndani yake na kujionyesha na mafakharisho, kinakuwa batili na anarudishiwa mwenye nacho. Isitoshe mwenye nacho anafikiwa badala yake anapata adhabu.

4- al-Kirmaaniy amesimulia maafikiano juu ya kwamba makusudio ya “kisimamo cha usiku” kwamba ni swalah ya tarawiyh. Fadhila hizi zinafikiwa kwa kule kusadikisha pia kisimamo hichi.

5- Hadiyth hii ni dalili juu ya fadhila za kisimamo cha Ramadhaan. Mapendekezo yake yamekokotezwa. Kuiswali swalah ya tarawiyh kwa mkusanyiko msikitini kumekokotezwa pia. Shaykh-ul-Islaam na wengine wamesema:

“Maswahabah walikuwa wakiitekeleza msikitini hali ya kutawanyika makundi kwa makundi wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hali akiwa anajua hilo na kuwakubalia. Mapokezi yamefahamisha juu ya kwamba kuswali tarawiyh kwa mkusanyiko ni bora kuliko kila mmoja kivyake. Hayo ni kwa maafikiano ya Maswahabah na watu wa mikao. Hayo vilevile ndio maoni ya wanachuoni wengi.”

6- Shaykh-ul-Islaam amesema:

“Swalah ambazo hazikusuniwa kuswaliwa kwa mkusanyiko uliyopangwa kama vile kisimamo cha usiku, sunnah za Rawaatib, swalah ya Dhuhaa, Tahiyyat-ul-Masjid na mfano wake inafaa kuziswali kwa mkusanyiko wakati fulani. Ama kuyachukulia hayo kuwa ni sunnah iliyopangwa ni Bid´ah iliyochukizwa.”

[1] al-Bukhaariy (2009) na Muslim (759).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdullaah bin ´Abdir-Rahmaan al-Bassaam
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tawdhwiyh-ul-Ahkaam min Buluugh-ul-Maraam, uk. (03/567-568)
  • Imechapishwa: 10/06/2017