01. Fadhilah za mwezi wa Ramadhaan


Ndugu wapendwa! Tumefikiwa na mwezi mkarimu na msimu mtukufu. Allaah ndani yake huongeza thawabu zilizokuwa nyingi na pia ndani yake hufungua milango ya kheri kwa kila mwenye kutaka. Ni mwezi wa kheri na baraka tele. Ni mwezi wa ruzuku na zawadi:

شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَىٰ وَالْفُرْقَانِ

“Mwezi wa Ramadhaan ambao imeteremshwa humo Qur-aan ili iwe mwongozo kwa watu na hoja bayana za mwongozo na pambanuo la batili.”[1]

Ni mwezi uliojaa rehema, msamaha, kuachwa huru na Moto ambao mwanzo wake ni rehema, katikati yake ni msamaha na mwisho wake ni kuachwa huru na Moto. Khabari zimetangaa juu ya fadhilah zake na kumepokelewa mapokezi mengi juu yake. al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Inapofika Ramadhaan basi hufunguliwa milango ya Pepo, hufungwa milango ya Moto na mashaytwaan hufungwa minyororo.”

Milango ya Pepo hufungwa kutokana na wingi wa matendo mema na kuwavutia watendaji. Milango ya Moto hufungwa kutokana na uchache wa maasi kutoka kwa waumini. Mashaytwaan hufungwa wasiweze kuyafanya yale wanayoweza kuyafanya wakati mwingine. Imaam Ahmad amepokea kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Ummah wangu wamepewa mambo matano katika Ramadhaan ambayo hawakupewa Ummah wowote miongoni mwa nyumati kabla yake: harufu ya mfungaji ni nzuri zaidi kuliko harufu ya miski, Malaika wanamuombea msamaha mpaka afungue swawm yake, Allaah kila siku anaipamba Pepo yake na anasema ”Waja wangu wema wanakaribia kuondolewa matatizo na maudhi na kuja Kwangu”, mashaytwaan waasi hufungwa minyororo na wanashindwa kuyafanya yale waliokuwa wanaweza kuyafanya wakati mwingine na wanasamehewa katika usiku wa mwisho.” Kukasemwa: ”Ee Mtume wa Allaah! Ni ule usiku wa makadirio?” Akasema: ”Hapana, lakini si vyenginevyo mtendaji hulipwa ujira wake anapomaliza kazi yake.”[2]

Ndugu wapendwa! Mambo haya matano Allaah ameyahifadhi kwa ajili yenu, amewahusu nyinyi kwayo kati ya nyumati zengine na akakuneemesheni kwayo ili akukamilishieni neema. Ni neema ngapi na fadhilah alizonazo Allaah juu yenu!

كُنتُمْ خَيْرَ أُمَّةٍ أُخْرِجَتْ لِلنَّاسِ تَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَتَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَتُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ

“Mmekuwa Ummah bora kabisa ulioteuliwa kwa watu: mnaamrisha mema na mnakataza maovu na mnamwamini Allaah.”[3]

[1] 02:185

[2] Ameipokea at-Twabaraaniy na al-Bayhaqiy katika ”ath-Thawaab” na cheni ya wapokezi wake ni dhaifu sana. Lakini baadhi ya mambo yana shawahidi Swahiyh.

[3] 03:110

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 08-09
  • Imechapishwa: 25/03/2020