01. Fadhilah za Dhikr


Allaah (Ta´ala) amesema:

فَاذْكُرُونِي أَذْكُرْكُمْ وَاشْكُرُوا لِي وَلَا تَكْفُرُونِ

“Basi nidhukuruni na Mimi nitakukumbukeni na nishukuruni wala msinikufuru.”[1]

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اذْكُرُوا اللَّـهَ ذِكْرًا كَثِيرًا

“Enyi walioamini!  Mdhukuruni Allaah kwa wingi wa kumdhukuru.”[2]

وَالذَّاكِرِينَ اللَّـهَ كَثِيرًا وَالذَّاكِرَاتِ أَعَدَّ اللَّـهُ لَهُم مَّغْفِرَةً وَأَجْرًا عَظِيمًا

“Wanaume wanaomdhukuru Allaah kwa wingi na wanawake [wanaofanya hivo], basi Allaah amewaandalia msamah na ujira mkubwa.”[3]

وَاذْكُر رَّبَّكَ فِي نَفْسِكَ تَضَرُّعًا وَخِيفَةً وَدُونَ الْجَهْرِ مِنَ الْقَوْلِ بِالْغُدُوِّ وَالْآصَالِ وَلَا تَكُن مِّنَ الْغَافِلِينَ

“Mdhukuru Mola wako katika nafsi yako kwa unyenyekevu na kwa khofu na si kwa kupaza sauti juu asubuhi na jioni na wala usiwe miongoni mwa walioghafilika.”[4]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mfano wa ambaye anamdhukuru Mola wake na ambaye hamdhukuru Mola wake ni kama mfano wa aliyehai na maiti.”[5]

“Je, nisikujulisheni bora ya matendo yenu, matakasifu zaidi mbele ya Mfalme, yaliyo juu katika daraja zenu, ambayo ni bora kwenu kuliko kutoa dhahabu na fedha, ambayo ni bora kwenu kuliko kukutana na adui zenu ambapo mkazikata shingo zao na wao wakazikata shingo zenu?” Wakasema: “Ndio, ee Mtume wa Allaah.” Akasema: “Kumdhukuru Allaah (Ta´ala).”[6]

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Allaah (Ta´ala) anasema: “Mimi niko vile mja Wangu anavyonidhania na Mimi ni pamoja Naye anaponitaja. Akinitaja kwenye nafsi yake Nami namtaja kwenye nafsi Yangu, akinitaja katika kundi, Nami namtaja katika kundi ambalo ni bora kuliko wao, akijikurubisha Kwangu paa moja Nami najikurubisha kwake dhiraa, akijikurubisha Kwangu dhiraa Nami najikurubisha kwake kwa kiasi cha kunyoosha mkono hadi kati ya kifuwa na akinijia kwa mwendo mdogo basi Mimi nitamjia kwa kuchapuka.”[7]

´Abdullaah bin Bashiyr (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia: “Kuna mtu alisema: “Ee Mtume wa Allaah!  Shari´ah za dini zimekuwa nyingi kwangu. Hivyo nielekeze katika kitu ambacho nitadumu nacho?” Akasema: “Usiache ulimi wako kuwa na unyevunyevu kwa kumdhukuru Allaah.”

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mwenye kusoma herufi moja kutoka katika Kitabu cha Allaah basi anapata thawabu za jema moja na jema moja linalipwa kwa kumi mfano wake. Sisemi: الم Alif, Laam, Miym ni herufi moja. Lakini “Alif” ni herufi moja, “Laam” ni herufi nyingine na “Miym” ni herufi nyingine.”

´Uqbah bin ´Aamir (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Alitoka Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na sisi tuko sehemu inayoitwa as-Swuffah akasema: “Ni nani kati yenu anayependa kila siku kuamkia Butwhaan au al-´Aqiyqi na aje na ngamia wawili walionenepa pasi na dhambi wala kukata udugu?” Tukasema: “Ee Mtume wa Allaah! Hakika tunapenda hilo.” Akasema: “Kwa nini asende mmoja wenu msikitini akajua na akasoma Aayah mbili kutoka katika Kitabu cha Allaah (´Azza wa Jall)? Hayo ni bora kwake kuliko kupata ngamia wawili, Aayah tatu ni bora kwake kuliko kupata ngamia watatu, Aayah nne ni bora kwake kuliko kupata ngamia wane na vivyo hivyo ni bora kuliko hesabu ya ngamia.”[8]

“Atakayekaa kikao ambapo hamtaji Allaah sehemu hiyo basi ana dhambi kutoka kwa Allaah na anayelala sehemu yoyote na asimtaje Allaah basi ana dhambi kutoka kwa Allaah.”[9]

“Hakuna watu wowote waliokaa sehemu na wasimtaje Allaah sehemu hiyo na wasimswalie Mtume wao isipokuwa wanapata dhambi; Allaah akitaka atawaadhibu na Akitaka atawasamehe.”[10]

“Hakuna watu wowote ambao watasimama sehemu waliokaa na wasimtaje Allaah hapo, basi watakuwa wamesimama kama mzoga wa punda na watakula khasara.”[11]

[1] 02:152

[2] 33:41

[3] 33:35

[4] 07:205

[5] al-Bukhaariy pamoja na al-Fath (11/208) kwa nambari. 6407, Muslim (01/539) kwa nambari. 779 kwa tamko lisemalo:

“Mfano wa nyumba ambayo kunatajwa Allaah ndani yake na nyumba ambayo hakutajwi Allaah ndani yake ni kama mfano wa aliyehai na maiti.” (01/539).

[6] at-Tirmidhiy (3377), Ibn Maajah (3790). Tazama “Swahiyh Ibn Maajah” (02/316) na “Swahiyh at-Tirmidhiy” (03/139).

[7] al-Bukhaariy (7405) na Muslim (2675) na a al-Bukhaariy.

[8][8] Muslim (803).

[9] Abu Daawuud (4856) na wengineo. Tazama “Swahiyh-ul-Jaami´” (05/342).

[10] at-Tirmidhiy (3380). Tazama “Swahiyh at-Tirmidhiy (03/140).

[11] Abu Daawuud (4855) na Ahmad (10680). Tazama “Swahiyh al-Jaami´” (05/176).

  • Mhusika: Shaykh Sa´iyd bin ´Aliy bin Wahf al-Qahtwaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Huswn-ul-Muslim
  • Imechapishwa: 09/06/2018