01. Dibaji ya “Min Usuwl ´Aqiydah Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah”

Himdi zote anastahiki Allaah, Mola wa walimwengu ambaye ametuongoza katika Uislamu:

وَمَا كُنَّا لِنَهْتَدِيَ لَوْلَا أَنْ هَدَانَا اللَّـهُ

“Na hatukuwa wenye kuongoka kama Allaah asingetuongoza.”[1]

Tunamuomba (Subhaanah) atuthibitishe juu yake mpaka wakati wa kufa kama alivyosema (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ حَقَّ تُقَاتِهِ وَلَا تَمُوتُنَّ إِلَّا وَأَنتُم مُّسْلِمُونَ

“Enyi mlioamini! Mcheni Allaah ukweli wa kumcha na wala msife isipokuwa nyinyi ni waislamu.”[2]

Asizipotoshe nyoyo zetu baada ya kuziongoza:

رَبَّنَا لَا تُزِغْ قُلُوبَنَا بَعْدَ إِذْ هَدَيْتَنَا

“Mola wetu usizipotoe nyoyo zetu baada ya kutuongoza.”[3]

Swalah na amani zimwendee Mtume wetu, kiigizo chetu na kipenzi chetu Muhammad ambaye ni Mtume wa Allaah aliyetuma hali ya kuwa ni rehema kwa walimwengu. Vilevile Allaah awawie radhi Maswahabah zake wema na wasafi ambao ni Muhaajiruun na Answaar na wale waliowafuata kwa wema daima.

Amma ba´d:

Haya ni maneno mafupi yenye kubainisha ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Lililopelekea kuiandika ni kutokana na yale Ummah wa Kiislamu hii leo unaeshi ndani yake katika mifarakano na tofauti vinavyowakilishwa na mapote na makundi mengi ya leo yenye kutofautiana. Kila mmoja anaita na kulitakasa kundi lake kiasi ambacho muislamu mjinga amekuwa ni mwenye kuchanganyikiwa na hajui ni nani anatakiwa kumfuata na kumuiga. Sivyo tu, bali hali imefikia kiasi ambacho kafiri anayetaka kusilimu hajui ni Uislamu upi ambao ni sahihi ambao aidha ameusoma au kuusikia na ambao umelinganiwa na Qur-aan na Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) uliowakilishwa na maisha ya Maswahabah watukufu na karne bora. Bali imekuwa mara nyingi anaona Uislamu bila ya waislamu – kama alivyosema Mustashriq[4] mmoja:

“Uislamu umeghaibiwa.”

Akimaanisha wale wenye kujinasibisha nao bila kusifika na uhakika wake. Lakini hata hivyo haina maana kuwa ni Uislamu kwa sura yake yote. Kwa kuwa Allaah (Subhaanah) amedhamini kuubakiza muda wa kubaki Kitabu Chake na kundi katika waislamu ambao wanautendea kazi, kuuhifadhi na kuutetea bado watakuwepo. Amesema (Ta´ala):

إِنَّا نَحْنُ نَزَّلْنَا الذِّكْرَ وَإِنَّا لَهُ لَحَافِظُونَ

“Hakika Sisi tumeteremsha Ukumbusho na hakika Sisi bila shaka ndio tutakaoihifadhi.”[5]

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا مَن يَرْتَدَّ مِنكُمْ عَن دِينِهِ فَسَوْفَ يَأْتِي اللَّـهُ بِقَوْمٍ يُحِبُّهُمْ وَيُحِبُّونَهُ أَذِلَّةٍ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ أَعِزَّةٍ عَلَى الْكَافِرِينَ يُجَاهِدُونَ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ وَلَا يَخَافُونَ لَوْمَةَ لَائِمٍ

“Enyi mlioamini! Yeyote atakayeritadi miongoni mwenu kutoka dini yake, basi Allaah ataleta watu atakaowapenda nao watampenda, wanyenyekevu kwa waumini na washupavu kwa makafiri; wanapambana Jihaad katika njia ya Allaah na wala hawakhofu lawama ya yeyote mwenye kulaumu.”[6]

وَإِن تَتَوَلَّوْا يَسْتَبْدِلْ قَوْمًا غَيْرَكُمْ ثُمَّ لَا يَكُونُوا أَمْثَالَكُم

“Mkikengeuka basi atabadilisha watu badala yenu kisha hawatokuwa mfano wenu.”[7]

Inahusiana na lile kundi ambalo Mtume mtukufu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema juu yake:

“Hakutoacha kuwepo kikundi katika Ummah wangu hali ya kuwa ni washindi. Hawatodhurika na wale wenye kuwanyima nusura na wenye kwenda kinyume nao mpaka kifike Qiyaamah ilihali bado wako katika hali hiyo.”[8]

Kuanzia hapa ni wajibu kwetu kulitambua kundi hili lililobarikiwa ambalo linauwakilisha Uislamu sahihi ili alitambue yule ambaye anautaka Uislamu sahihi na watu wake wa uhakika ili aweze kuwaiga na vilevile wajiunge nao wale makafiri wanaotaka kuingia katika Uislamu. Tunamuomba Allaah atujaalie kuwa katika kundi hilo.

[1] 07:43

[2] 03:102

[3] 03:08

[4] Tazama https://firqatunnajia.com/nini-الاستشراق-na-المستشرقين/

[5] 15:09

[6] 05:54

[7] 47:38

[8] al-Bukhaariy (7311), Muslim (5059), Abu Daawuud (4654), at-Tirmidhiy (6669), Ibn Maajah (06) na Ahmad (04/97).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Min Usuwl ´Aqiydah Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 03-06
  • Imechapishwa: 12/05/2022