Himdi zote anastahiki Allaah ambaye ameifaradhisha swalah kwa waja Wake na akawaamrisha kuitekeleza ipasavyo. Amefungamanisha kuokoka na kufaulu kwa kule kuwa na unyenyekevu katika swalah na akaifanya kuwa ni kigezo cha kupambanua kati ya kufuru na imani na kinga dhidi ya machafu na maovu.

Swalah na salamu zimwendee Mtume wetu Muhammad aliyezungumzishwa Naye (Ta´ala):

وَأَنزَلْنَا إِلَيْكَ الذِّكْرَ لِتُبَيِّنَ لِلنَّاسِ مَا نُزِّلَ إِلَيْهِمْ

“Tumekuteremshia Ukumbusho ili uwabainishie watu yaliyoteremshwa kwao.”[1]

Hivyo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akatekeleza kazi hii vilivyo. Swalah ilikuwa ni miongoni mwa mambo muhimu kabisa ambayo aliyabainisha kwa kuieleza kimaneno na kimatendo. Kiasi cha kwamba kuna siku aliswali akiwa juu ya mimbari. Akasimama juu yake, akaenda katika Rukuu´ na akasema kuwaambia:

“Enyi watu! Nimefanya hivi ili mnifuate na mjifunze swalah yangu.”[2]

Ametuwajibishia (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuswali kama anavoswali yeye kwa kusema:

“Swalini kama mlivyoniona nikiswali.”[3]

Amembashiria (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa kumuahidi yule mwenye kuswali kama atakavyoswali basi atamwingiza Peponi kwa kusema:

“Allaah (´Azza wa Jall) amefaradhisha swalah tano. Mwenye kutawadha vizuri ipasavyo, akaswali kwa nyakati zake na akatimiza Rukuu´ zake, Sujuud zake na akanyenyekea basi ana ahadi kwa Allaah kwamba atamsamehe. Yule asiyeyafanya hayo, basi hana ahadi kwa Allaah kwamba atamsamehe; Akitaka kumsamehe, atamsamehe, na akitaka kumuadhibu, atamuadhibu.”[4]

Swalah na salamu ziwaendee vilevile jamaa zake na Maswahabah zake ambao ni wachaji na wema (ambao wametunakilia ´ibaadah zake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), swalah zake, maneno yake na vitendo vyake na wakayafuata) na wale wengine wote ambao watawafuata na kupita juu ya njia yao mpaka siku ya Qiyaamah.

[1] 16:44

[2] al-Bukhaariy na Muslim.

[3] al-Bukhaariy, Muslim na Ahmad. Imetajwa katika ”Irwaa’-ul-Ghaliyl” (213).

[4] Hadiyth ni Swahiyh na imesahihishwa na maimamu wengi. Nimeiweka katika ”Swahiyh Sunan Abiy Daawuud” (451) na (1276).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 33-35
  • Imechapishwa: 15/01/2019