01. Dibaji


Himdi zote zinamstahikia Allaah. Tunamhimidi Yeye na kumuomba msaada na msamaha. Tunajilinda Kwake kutokamana na shari ya nafsi zetu na uovu wa matendo yetu. Yule mwenye kuhidiwa na Allaah, basi hakuna wa kumpoteza, na yule mwenye kupotezwa Naye, basi hakuna wa kumuhidi.

Nashuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah, hali ya kuwa hana mshirika, na ninashuhudia ya kwamba Muhammad ni mja na ni Mtume Wake – swalah na salaam zimwendee yeye, kizazi chake na Maswahabah zake.

Amma ba´d:

Hakika ya Allaah (Ta´ala) amemtuma Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa uongofu na dini ya haki awe ni rehema kwa walimwengu na kiigizo kwa watendaji na hoja kwa waja wote. Ametekeleza amana, akafikisha ujumbe, akaunasihi Ummah na akawabainishia watu yale yote wanayoyahitajia ya misingi na matawi ya dini. Hakuacha kheri yoyote, isipokuwa amewabainishia nayo na kuwasisitiza kwayo. Hakuacha shari yoyote ile isipokuwa ameutahadharisha Ummah nayo. Ameuacha Ummah katika njia nyeupe ambayo usiku wake ni kama mchana wake. Katika njia hii ya kung´ara na kumeremeta wakapita Maswahabah zake. Vilevile wakaipokea njia hii wale wengine wa karne tukufu.

Namna wakati ulivyokuwa ukienda mazingira yakaingiliwa na Bid´ah mbali mbali. Hizi zilikuwa ni njama za wazushi dhidi ya Uislamu na waislamu. Wakawa wakizama kwenye Bid´ah na wakijenga I´tiqaad zao kwenye utando wa buibui. Pamoja na hivyo Mola (Ta´ala) anailinda dini Yake kwa mawalii Wake ambao amewatunukia imani, elimu na hekima ambavyo kwavyo wanawatandika maadui hawa na vitimbi vyao. Hakuna mtu yeyote ambaye alizusha Bidah, isipokuwa Allaah – na himdi zote ni za Allaah – alifanya kupatikana kwa mtu katika Ahl-us-Sunnah ambaye anairaddi na kuifichukua Bid´ah yake.

Miongoni mwa wale waliosimama msitari wa mbele kabisa dhidi ya watu wa Bid´ah hawa ni Shaykh-ul-Islaam Taqiyy-ud-Diyn Ahmad bin ´Abdil-Haliym bin ´Abdis-Salaam bin Taymiyyah al-Haraaniy ad-Dimashqiy. Alizaliwa Jumatatu tarehe kumi Rabi´-ul-Awwal 661 na alifariki kwa kutiwa jela na kwa kudhulumiwa Damaskus Dhul-Qa´dah 728 – Allaah amrehemu. Ana vitabu vingi ambapo amebainisha Sunnah na kukomaza nguzo zake na kuponda Bid´ah.

Moja katika vitabu vyake katika maudhui haya ni “al-Fatwaa al-Hamawiyyah” alichokiandika 698 ikiwa ni jibu la swali aliloulizwa kutoka Hamaah, Syria. Mtu huyo alikuwa akiuliza ni upi msimamo wa wanachuoni na maimamu juu ya Aayah na Hadiyth za sifa za Allaah. Akajibu kwa jibu lililokuwa na kurasa 83. Kwa sababu ya jibu hili akasibiwa na mitihani na matatizo. Allaah amjaze kheri kwa Uislamu na waislamu.

Ilipokuwa wasomaji wengi wana uzito wa kuelewa na kulifahamu jibu hili, nikapendelea kufupisha yale mambo muhimu zaidi na kuweka nyongeza zinazohitajika. Kitabu nimekipa jina ”Fath Rabb-il-Bariyyah bi Talkhiys-il-Hamawiyyah”.

Nilikichapisha mara ya kwanza mwaka wa 1380. Hivi tena ninakichapisha kwa mara ya pili. Kuna uwezekano nimebadilisha kitu kwa minajili ya manufaa.

Ninamuomba Allaah ajaalie matendo yetu yawe ni yenye kufanywa kwa ajili Yake Pekee na yawanufaishe waja Wake – hakika Yeye ni Mwingi wa kutoa na ni mkarimu.