01. Ndio maana somo la ´Aqiydah likawa muhimu

Kwa jina la Allaah, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu

Himdi zote anastahiki Allaah, Mola wa walimwengu. Swalah na amani zimwendee Mtume wetu Muhammad, ambaye ndiye Nabii wa mwisho na kiongozi wao ambaye ametumwa akiwa ni rehema kwa walimwengu. Amefikisha ujumbe, akatekeleza amana, akaunasihi Ummah, akapambana Jihaad katika njia ya Allaah ukweli wa kupambana. Kupitia kwake Allaah akaikamilisha dini na akaitimiza neema. Amewawajibishia viumbe kumtii na kumfuata. Vilevile amewawajibishia kumpenda zaidi kuliko wanavyojipenda wao wenyewe, wazazi wao, watoto wao na watu wote kwa jumla.

Amma ba´d:

Tutazungumzia mada ambayo inamuhusu kila muislamu, mwanaume na mwanamke. Nayo si nyengine ni kuhusu ´Aqiydah. ´Aqiydah ndio msingi sahihi unaojengewa juu yake matendo yote. Kila kitendo ambacho hakikujengwa juu ya ´Aqiydah sahihi ni chenye kurudishwa kwa yule mtendaji. Haijalishi namna atavyojitaabisha nafsi yake na kutumia maisha yake katika kitendo hicho.

´Aqiydah ndio msingi wa dini na ndio ulinganizi wa Manabii na Mitume, kuanzia wa mwanzo wao mpaka wa mwisho wao. ´Aqiydah ndio kitu cha kwanza atachoulizwa mja siku ya Qiyaamah. Imethibiti katika Athar:

“Kuna maneno mawili watayoulizwa wa mwanzo na wa mwisho wao: Ni kipi mlichokuwa mnaabudia? Ni kipi mlichowajibu Wajumbe?”

Maswali haya mawili wataulizwa viumbe wote siku ya Qiyaamah.

Jibu ya swali la kwanza ni “Kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah.

Jibu ya swali la pili ni “Kushuhudia ya kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah” kwa kuyatamka na kuyatendea kazi.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mujmal ´Aqiydat-is-Salaf as-Swaalih, uk. 02
  • Imechapishwa: 24/05/2022