Himdi zote kamilifu zinamstahikia Allaah, Mola wa walimwengu. Swalah na salaam ziwe juu ya Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah wake wote.

Amma ba´d:

Hakika ´Aqiydah ndio msingi wa dini, ambayo ni ile ´Aqiydah sahihi iliyojengeka juu ya Qur-aan na Sunnah. Ndio asili na msingi wa dini. ´Aqiydah ikiwa sahihi na ikasalimika na yanayoiharibu au yenye kuitia kasoro, hivyo hakika mambo mengine yaliyobaki ya dini yatajengeka juu yake. Ama ´Aqiydah ikiharibika, kutakuwa hakuna faida ya matendo. Wala dini haiwezi kusimama isipokuwa kwa ´Aqiydah sahihi iliyojengeka juu ya Qur-aan na Sunnah za Mtume Wake na kwa mujibu wa yale waliyokuwemo Salaf wa Ummah huu; katika Maswahabah, Taabi´iyn na wale waliowafuata katika maimamu na wale walinganizi wanaolingania katika dini ya Allaah (´Azza wa Jall). Kwa ajili hii kitu cha kwanza walichoanza nacho Mitume wakati wa kulingania kwao ilikuwa ni kuzisahihisha ´Aqiydah. Mitume wote kitu cha kwanza walichokuwa wakiwaambia watu wao:

قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ

“Enyi watu wangu! Mwabuduni Allaah, kwani hamna nyinyi mwabudiwa wa haki asiyekuwa Yeye.” (07:59)

Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ambaye ndiye Nabii wa mwisho na kiongozi wa Mitume wote, pindi Allaah (´Azza wa Jall) alipomtuma kulingania katika dini ya Allaah, kitu cha kwanza alichoanza nacho ilikuwa ni kuzisafisha ´Aqiydah. Akawa anawaita watu kumpwekesha (Jalla wa ´Alaa) kwa kumuabudu na kuacha kuabudu asiyekuwa Yeye katika masanamu, miti, mawe, waliohai na vyenginevyo katika viumbe.

Alibaki Makkah miaka 13 akiwalingania watu kumpwekesha Allaah na  kuitengeneza ´Aqiydah. Ilikuwa ni kabla ya kufaradhishiwa Swalah, Zakaah, Swawm na Hajj. Ni katika dalili inayofahamisha ya kwamba matendo haya hayasihi isipokuwa tu pale yatapokuwa yamejengeka juu ya ´Aqiydah sahihi. Nayo ni kumpwekesha Allaah (Jalla wa ´Alaa) kwa ´ibaadah na kuacha kuabudia asiyekuwa Yeye. Hili ndilo lengo la Allaah kuwaumba viumbe kwa ajili yake. Amesema (Ta´ala):

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ

“Na Sikuumba majini na watu isipokuwa waniabudu.” (51:56)

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Haki ya Allaah juu ya waja Wake wamuabudu na wala wasimshirikishe Yeye na chochote.”

“Haki ya waja kwa Allaah asimuadhibu yule ambaye hakumshirikisha Yeye na chochote.”

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-´Aqiydah al-Islaamiyyah as-Swahiyhah https://www.youtube.com/watch?v=KqoTCYds6Cs&t=13s
  • Imechapishwa: 27/05/2017