01. Adabu ya kwanza: kumtakasia nia Allaah

Ni wajibu kumtakasia nia Allaah (´Azza wa Jall) katika kila ´amali. Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) amesema:

“Kama jinsi ni mungu mmoja hakuna mungu wa haki asiyekuwa Yeye kadhalika inatakiwa ´ibaadah zote afanyiwe Yeye Pekee, hali ya kuwa mmoja hana mshirika. Kama Alivyopwekeka katika uungu basi ni wajibu apwekeshwe katika ´ibaadah. Matendo mema ni yale yaliyotakasika kutokana na riyaa yaliyofungamanishwa na Sunnah.”

Amesema katika “Taysiyr-ul-´Aziyz al-Hamiyd”[1]:

“Mambo haya mawili ndio nguzo za matendo yenye kukubaliwa. Hivyo ni lazima yawe ya sawa na yatakasike. Ya sawa ni yale yenye kuafikiana na Sunnah nayo ni yale yaliyoashiriwa katika maneno Yake (Ta´ala):

فَلْيَعْمَلْ عَمَلًا صَالِحًا

“Afanye ‘amali njema… “

Yaliyotakasika ni yale yenye kutakasika na shirki ya wazi na iliyojificha nayo ni ile iliyoashiriwa katika maneno Yake:

وَلَا يُشْرِكْ بِعِبَادَةِ رَبِّهِ أَحَدًا

“… na wala asishirikishe katika ‘ibaadah za Mola wake yeyote.” (18:110)

Ni lazima kwa mtafutaji wa elimu aifanye nia yake kuwa nzuri katika kuitafuta kwake. Kuifanya nia kuwa nzuri kunakuwa kumkusudia kwayo Uso wa Allaah (Ta´ala), kuitendea kazi, kuhuisha Shari´ah, kuutia moyo wake nuru, kujikurubisha kwa Allaah siku ya Qiyaamah na kutamani vile alivyowaandalia watu wake katika radhi na fadhila Zake kuu. Sufyaan ath-Thawriy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Sikupambana na kitu kigumu kwangu kuliko nia yangu.”

Katika kutafuta kwake elimu asikudie mambo ya kidunia katika kufikia uongozi, heshima, mali, kutaka watu wamtukuze na kutaka aonekane katika vikao na mfano wa hayo. Hivyo akawa ni mwenye kubadilisha kilicho duni kwa kiliko na kheri zaidi.

[1] Uk. 525.

  • Mhusika: Shaykh Muhammad Sa´iyd Raslaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Aadab Twaalib-ul-´Ilm, uk. 23-24
  • Imechapishwa: 23/04/2017