00. Utangulizi wa Shaykh Rabiy´ al-Madkhaliy juu ya kitabu “al-Baraahiyn al-Injiyliyyah”

Himdi zote anastahiki Allaah. Swalah na salaam zimwendee Mtume wa Allaah, kizazi chake, Maswahabah wake na wale wataofuata mwongozo wake.

Amma ba´d:

Hakika kijitabu hiki kwa anwani “al-Baraahiyn al-Injiylyyah ´alaa anna ´Iysaa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) daakhil fiyl-´Ubuudiyyah wa la hadhdhwa lahu fiyl-Uluuhiyya” cha mwandishi ´Allaamah Taqiyy-ud-Diyn al-Hilaaliy – pamoja na udogo wake ni miongoni mwa vitabu bora vilivyoandikwa vikiwarradi manaswara na kuthibitisha kuwa ´Iysaa ni mja na ni Mtume wa Allaah, kama walivyo Mitume wengine wote, na kwamba sio mwana wa Allaah – Ametakasika Allaah kutokamana na yale wanayoyasema! Shaykh Taqiyy-ud-Diyn amethibitisha hayo kutoka kwenye maandiko ya Injili. Amefanya hivo kwa njia ya wazi kabisa. Hakuna atayepinga hilo isipokuwa mwenye kiburi.

Lau isingelikuwa ni kwa sababu ya kiburi na ukaidi basi manaswara wengi wangejirudi na wakaingia katika dini ya haki ya Uislamu ambayo inamsifu Mtume wa Allaah ´Iysaa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kumfanya ni mmoja katika wale Mitume bora (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam).

Katika Uislamu hakuna chochote kinachowafanya manaswara na wengineo kuwa na uadui dhidi ya Uislamu unaowapa Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) – akiwemo Muusa na ´Iysaa – nafasi yao stahiki. Si chengine kinachowafanya hivo isipokuwa ni ushabiki wa kipofu.

Qur-aah hii ambayo majini na watu wameshindwa kuleta mfano wake, Sura ishirini mfano wake au Sura moja mfano wake, inalingania katika uhalisia huu na kuwalinda wale ambao Allaah anawatakia kheri kuiamini, kuitukuza, kuiadhimisha na kuamini zile I´tiqaad na Shari´ah zenye heshima ilizokuja nazo. Vilevile inalingania katika kuwaheshimu Manabii na Mitume, uadilifu, inswafu, huruma na inalingania katika kila kheri na inaonya kila shari:

إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَذِكْرَىٰ لِمَن كَانَ لَهُ قَلْبٌ أَوْ أَلْقَى السَّمْعَ وَهُوَ شَهِيدٌ

“Hakika katika hayo bila shaka ni ukumbusho kwa yule mwenye moyo au akatega sikio naye akawa ni mwenye kufahamu.” (50:37)

Vilevile napenda kukumbusha kuwa kumeandikwa vitabu vingi vinavyowalingania manaswara na mayahudi katika Uislamu na kubainisha ule upotevu na mageuzo yaliyoingizwa katika Taurati na Injili. Haya ni mambo ambayo yanawaita wale wenye busara, ambao wanataraji radhi za Allaah, kuogopa ghadhabu na adhabu Yake kali ambazo zinasababisha kudumu Motoni milele, kuingia katika Uislamu. Miongoni mwa vitabu hivyo ni vifuatavyo:

1- “al-Jawaab as-Swahiyh liman baddala diyn al-Masiyh” cha Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah. Ameandka mijaladi 6.

2- “Hidaayat-ul-Hayaaraa fiy ajwibat al-Yahuud wan-Naswaaraa” cha Ibn-ul-Qayyim al-Jawziy. Ni kitabu ndogo lakini chenye hadhi kubwa.

3- “Idhwhaar-ul-Haqq” cha Rahmatullaah al-´Uthmaan al-Hindiy. Ni mujaladi mbili lakini hata hivyo ndani yake mna kasoro fulani.

4- “al-Hisaam al-Mamduud fiyr-Radd ´alaa al-Yahuud” cha ´Abdul-Haqq al-Islaamiy al-Maghribiy. Ni mujaladi ndogo.

Ninamuomba Allaah awanufaishe waislamu, mayahudi na manaswara kwa juhudi hizi, awazidishie waislamu elimu na ujuzi kupitia juhudi hizi na awafanye mayahudi na manaswara kuwa na mazingatio, uadilifu, kuuheshimu Uislamu, kuuamini na kuufuata.

Imeandikwa na Rabiy´ bin Haadiy ´Umar al-Madkhaliy

15-10-1431