00. Dibaji ya “Tabswiyr-ul-Anaam bisharh Nawaaqidh-il-Islaam”

Himdi zote njema zinamstahikia Allaah, Mola wa walimwengu. Swalah na amani zimwendee Nabii na Mtume bora kabisa Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake wote.

Ama baada ya haya; 

Huu ni ufafanzui wa kitabu “Nawaaqidh-ul-Islaam” kilichokusanywa  na Imaam na Shaykh na Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah). Haya ndio mambo kumi muhimu zaidi yanayochengua Uislamu.

Vichenguzi ni wingi wa kichenguzi. Kichenguzi maana yake ni kitu chenye kubatilisha na kuharibu. Mambo yenye kuchengua Uislamu maana yake ni mambo yenye kuuharibu na kuubatilisha Uislamu. Kwa msemo mwingine ina maana ya kwamba mtu akifanya moja katika mambo haya Uislamu na dini yake vinabatilika. Matokeo yake anatoka katika dini ya Uislamu na kwenda katika dini ya waabudia masanamu. Badala ya kuwa muislamu anakuwa mwabudia masanamu. Isipokuwa ikiwa kama atatubu kabla ya kufa. Asipotubu kabla ya kufa baada ya kufanya moja katika mambo haya, basi anatoka katika Uislamu na anakuwa mwabudia masanamu. 

Kwa hivyo vichenguzi maana yake ni mambo yenye kubatilisha na kuharibu. Ni kama mfano wa vichenguzi vya wudhuu´. Moja katika mambo hayo ni chenye kutoka kupitia ima tupu ya mbele au tupu ya nyuma. Mtu akitawadha kisha akatokwa na mkojo au kinyesi, basi wudhuu´ wake unabatilika na kuharibika. Hivyo anatoka katika hali ya kuwa na wudhuu´ na kwenda katika hali ya hadathi. Vivyo hivyo vichenguzi vya Uislamu. Mtu atapofanya moja katika mambo haya yenye kuchengua Uislamu anatoka katika Uislamu na kwenda katika waabudia masanamu.

Uislamu maana yake ni kujisalimisha kwa Allaah pekee kwa kumpwekesha na kumwabudu. Tawhiyd ni kumpwekesha Allaah kwa kumwabudu pekee. Amesema (Ta´ala):

وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاءَ وَيُقِيمُوا الصَّلَاةَ وَيُؤْتُوا الزَّكَاةَ ۚ وَذَٰلِكَ دِينُ الْقَيِّمَةِ

“Hawakuamrishwa jengine isipokuwa wamwabudu Allaah hali ya kumtakasia Yeye dini kwa kujiengua na shirki na kuelemea Tawhiyd, na wasimamishe swalah na watoe zakaah – na hiyo ndiyo dini iliyosimama imara.”[1]

´Ibaadah ni kila kilichotajwa na Shari´ah katika maamrisho na makatazo. Kila kilichoamrishwa na Mweka Shari´ah katika maamrisho kwa njia ya kulazimisha au kupendezesha, au akakataza kwa njia ya uharamu au ya machukizo.

Mtu atapofanya moja katika mambo haya kumi yenye kuchengua Uislamu aliyotaja mtunzi ndani ya kitabu chake hiki, basi anatoka katika Uislamu na kwenda katika waabudia masanamu. Tunamuomba Allaah usalama.

Imaam (Rahimahu Allaah) amefupisha juu ya haya mambo kumi kwa sababu ndio mambo muhimu zaidi yenye kuchengua Uislamu. Sababu nyingine ni kwa kuwa mambo mengi yanayochengua Uislamu yanarejea katika mambo kumi haya.

[1] 98:05

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tabswiyr-ul-Anaam bisharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 05-06