00. Dibaji ya kitabu “´al-Aqiydah as-Swahiyhah”

Himdi zote njema anastahiki Allaah. Swalah na amani zimwendee yule ambaye hakuna Mtume mwingine baada yake, kizazi chake na Maswahabah wake.

Ama baada ya hayo;

Pale ilipokuwa ´Aqiydah sahihi ndio asili na msingi wa Uislamu, ndipo nikaonelea iwe maudhui ya muhadhara. Ni jambo linalojulikana kupitia dalili za Kishari´ah kutoka katika Qur-aan na Sunnah ya kwamba maneno na matendo yanakubaliwa tu pale yatapokuwa ni yenye kutoka katika ´Aqiydah sahihi. ´Aqiydah ikiwa sio sahihi, basi yale matendo na maneno yaliyojengwa juu yake yanabatilika. Amesema (Ta´ala):

وَمَن يَكْفُرْ بِالْإِيمَانِ فَقَدْ حَبِطَ عَمَلُهُ وَهُوَ فِي الْآخِرَةِ مِنَ الْخَاسِرِينَ

“Na yeyote atakayekufuru imani, basi hakika yamebatilika matendo yake – naye Aakhirah atakuwa miongoni mwa waliokhasirika.” (05:05)

وَلَقَدْ أُوحِيَ إِلَيْكَ وَإِلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكَ لَئِنْ أَشْرَكْتَ لَيَحْبَطَنَّ عَمَلُكَ وَلَتَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ

“Hakika umefunuliwa Wahy wewe na kwa wale waliokuwa kabla yako ya kwamba ukifanya shirki bila shaka yatabatilika matendo yako na [Aakhirah] utakuwa miongoni mwa waliokhasirika.” (39:65)

Kuna Aayah nyingi zikiwa na maana kama hii.

Kitabu cha Allaah na Sunnah za Mtume Wake mwaminifu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) vimefahamisha kuwa ´Aqiydah sahihi imefupishwa katika kumuamini Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Wake, siku ya Mwisho na makadirio ya kheri na ya shari. Mambo haya sita ndio misingi ya ´Aqiydah sahihi ambayo imeteremshwa na Kitabu cha Allaah kitukufu na Allaah akamtuma kwayo Mtume Wake Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Misingi hii inatoa matawi kila kile ambacho ni wajibu kukiamini katika mambo yaliyofichikana na mambo yote yaliyoelezwa na Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Dalili ya misingi hii katika Qur-aan na Sunnah ni nyingi sana. Miongoni mwazo ni maneno ya Allaah (Subhaanah):

لَّيْسَ الْبِرَّ أَن تُوَلُّوا وُجُوهَكُمْ قِبَلَ الْمَشْرِقِ وَالْمَغْرِبِ وَلَـٰكِنَّ الْبِرَّ مَنْ آمَنَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ وَالْمَلَائِكَةِ وَالْكِتَابِ وَالنَّبِيِّينَ

“Si wema pekee kuelekeza nyuso zenu upande wa mashariki na magharibi, lakini wema khaswa ni anayemuamini Allaah na siku ya Mwisho na Malaika na Kitabu na Manabii.” (02:177)

آمَنَ الرَّسُولُ بِمَا أُنزِلَ إِلَيْهِ مِن رَّبِّهِ وَالْمُؤْمِنُونَ ۚ كُلٌّ آمَنَ بِاللَّـهِ وَمَلَائِكَتِهِ وَكُتُبِهِ وَرُسُلِهِ لَا نُفَرِّقُ بَيْنَ أَحَدٍ مِّن رُّسُلِهِ

“Mtume ameamini yaliyoteremshwa kwake kutoka kwa Mola wake na waumini [pia wameamini]. Wote wamemwamini Allaah na Malaika Wake na Vitabu Vyake na Mitume Yake; [nao husema]: “Hatutafautishi baina ya yeyote kati ya Mitume Yake.” (02:285)

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا آمِنُوا بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ وَالْكِتَابِ الَّذِي نَزَّلَ عَلَىٰ رَسُولِهِ وَالْكِتَابِ الَّذِي أَنزَلَ مِن قَبْلُ ۚ وَمَن يَكْفُرْ بِاللَّـهِ وَمَلَائِكَتِهِ وَكُتُبِهِ وَرُسُلِهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا بَعِيدًا

“Enyi mlioamini! Mwaminini Allaah na Mtume Wake na Kitabu alichokiteremsha kwa Mtume Wake na Kitabu alichokiteremsha hapo kabla. Yeyote atakayemkufuru Allaah na Malaika Wake na Vitabu Vyake na Mitume Yake na siku ya Mwisho, basi hakika amepotoka upotofu wa mbali kabisa.” (04:136)

أَلَمْ تَعْلَمْ أَنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُ مَا فِي السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ ۗ إِنَّ ذَٰلِكَ فِي كِتَابٍ ۚ إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ

“Je, hujui kwamba Allaah anajua yale yote yaliyomo mbinguni na ardhini? Hakika hayo yamo ndani ya Kitabu, hakika hayo kwa Allaah ni mepesi.” (22:70)

Kuhusu dalili sahihi zenye kuthibitisha misingi hii ni nyingi sana. Miongoni mwazo ni Hadiyth Swahiyh inayojulikana ambayo Muslim ameipokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa kiongozi wa waumini ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesimulia kuwa Jibriyl (´alayhis-Salaam) alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu imani ambapo akasema:

“Imani ni kumuamini Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Wake, siku ya Mwisho na kuamini makadirio ya kheri na ya shari.”[1]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa Abu Hurayrah.

Misingi hii inatoa matawi ya kila kile ambacho ni wajibu kwa muislamu kukiamini juu ya Allaah (Subhaanah), mambo ya siku ya Qiyaamah na mambo mengine yaliyofichikana.

[1] Muslim (08), at-Tirmidhiy (2610), an-Nasaa´iy (4990), Abu Daawuud (4695), Ibn Maajah (63) na Ahmad (01/27).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-´Aqiydah as-Swahiyhah wa maa yudhwaadduhaa, uk. 03-04
  • Imechapishwa: 24/05/2023