وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ – مسجد الإرشاد

  Download

Sehemu ya kwanza

Himdi zote njema anastahiki Allaah. Tunamhimidi Yeye, tunamuomba msaada na tunamuomba msamaha. Tunajilinda kwa Allaah kutokamana na shari ya nafsi zetu na matendo yetu maovu. Yule aliyeongozwa na Allaah, hakuna wa kumpoteza, na ambaye amepotezwa na Allaah, hakuna wa kumwongoza. Nashuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah, hali ya kuwa yupeke yake hana mshirika, na nashuhudia ya kwamba Muhammad ni mja na Mtume Wake.

Hakika mazungumzo bora kabisa ni maneno ya Allaah. Uongofu bora ni wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mambo maovu kabisa ni yale yaliyozuliwa. Kila kilichozuliwa ni Bid´ah. Kila Bid´ah ni upotevu. Kila upotevu ni Motoni.

Amma ba´d:

Ndugu zangu wapendwa kwa ajili ya Allaah! Hakika Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) hakutuumba katika dunia hii isipokuwa kwa ajili ya heshima kubwa na lengo tukufu. Nalo si lingine ni kumwabudu Allaah, hali ya kuwa yupekee hana mshirika:

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ

“Sikuumba majini na watu wa isipokuwa waniabudu.” (adh-Dhaariyaat 51:52)

Sisi katika maisha haya tumeamrishwa tuzielekeze ´ibaadah kwa Allaah Mmoja, Aliye juu kabisa na wala tusimshirikishe Yeye na chochote. Tuyaelekeze mambo yetu yote, kuishi na kufa kwetu kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala):

قُلْ إِنَّ صَلَاتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ

”Sema: “Hakika swalah yangu na kichinjwa changu na uhai wangu na kufa kwangu ni kwa ajili ya Allaah pekee.” (al-An´aam 06:162-163)

Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) anawapa majaribio na mitihani waja Wake ili kuona kama ni wenye kutii na wenye kuelekea kwa Mola wa ardhi na mbingu na kama watampwekesha Allaah (´Azza wa Jall) kwa ´ibaadah au ni kinyume na hivo. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amewatahini waja katika dunia hii wanapokuwa katika njia yao ya kwenda kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) kwa mikingamo mitatu inayomzuia mja kutofika kwa Mola Wake, inamzuia mja kutofika katika kufaulu na inamzuia mja kutofika kwenye Pepo yenye neema mbalimbali.

Waja wa Allaah! Mikingamo hii mitatu mkubwa na wenye khatari zaidi ni kumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Njia ya kusalimika nayo ni kumpwekesha Allaah (´Azza wa Jall) kwa Tawhiyd.

Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ametutahadharisha kutokamana na shirki, akabainisha mwisho wa watu wake, ukali wa adhabu yao na kwamba yule atakayekuja na shirki kubwa basi atadumishwa ndani ya Moto milele:

إِنَّهُ مَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدْ حَرَّمَ اللَّـهُ عَلَيْهِ الْجَنَّةَ وَمَأْوَاهُ النَّارُ ۖ وَمَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ أَنصَارٍ

“Hakika yule atakayemshirikisha Allaah, basi hakika Allaah atamharamishia Pepo na makazi yake yatakuwa ni motoni – na madhalimu hawatopata yeyote mwenye kuwanusuru.” (al-Maaidah 05:72)

Yule atakayemwendea Allaah na shirki kubwa basi Allaah (´Azza wa Jall) hatomsamehe na atakuwa ni mwenye kudumishwa Motoni milele:

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ

“Hakika Allaah hasamehi kushirikishwa na anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa amtakae.” (an-Nisaa´ 04:48)

Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ameifanya shirki ndio dhambi kubwa na dhuluma kubwa:

إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ

“Hakika shirki ni dhulma kubwa mno!” (Luqmaan 31 : 13)

Allaah (´Azza wa Jall) amewaamrisha Mitume wote iwe kitu cha kwanza wanachowaamrisha watu wao na kuwaita kwacho ni ulinganizi katika Tawhiyd ya Allaah na kutahadharisha kutomshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala):

وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِي كُلِّ أُمَّةٍ رَّسُولًا أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ وَاجْتَنِبُوا الطَّاغُوتَ

“Hakika Tulituma katika kila ummah Mtume [awaamrishe watu wake] kwamba: “Mwabuduni Allaah na jiepusheni na Twaaghuut.” (an-Nahl 16 : 32)

Ametuamrisha (Subhaanahu wa Ta´ala) tusielekeze ´ibaadah kwa mwengine isipokuwa kwa Allaah Mmoja asiyekuwa na mshirika:

وَلَا تَدْعُ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَنفَعُكَ وَلَا يَضُرُّكَ ۖ فَإِن فَعَلْتَ فَإِنَّكَ إِذًا مِّنَ الظَّالِمِينَ

“Wala usiombe badala ya Allaah asiyekufaa na wala asiyekudhur; na ukifanya hivyo, basi hakika utakuwa miongoni mwa madhalimu.” (Yuunus 10:106)

Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amekata mizizi ya shirki, akakataza aina zake zote, akakataza njia zake zote na akatahadharisha (Subhaanahu wa Ta´ala) na Mtume wetu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) vilevile akatahadharisha kutokamana na shirki kubwa na shirki ndogo. Kuhusu shirki kubwa ni kule kumuomba mwengine asiyekuwa Yeye (´Azza wa Jall) na kuzielekeza ´ibaadah kwa asiyekuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Hivyo hatumuombi mwengine isipokuwa Allaah (´Azza wa Jall):

وَأَنَّ الْمَسَاجِدَ لِلَّـهِ فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّـهِ أَحَدًا

“Sehemu zote za kuswalia ni kwa ajili ya Allaah, hivyo basi msiombe yeyote pamoja na Allaah.” (al-Jinn 72:18)

Hatumwabudu mtu yeyote, hatumwabudu kiumbe yeyote; hatumuombi Malaika aliyekaribu wala Mtume aliyetumilizwa. Bali tunaelekeza du´aa na maombi yetu kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala):

وَقَالَ رَبُّكُمُ ادْعُونِي أَسْتَجِبْ لَكُمْ

”Mola wenu amesema: “Niombeni Nitakuitikieni.” (Ghaafir 40:60)

Hakusema tuwaombe waliyomo ndani ya makaburi wala waliohai badala ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Bali zielekezeni du´aa na maombi yenu kwa Allaah Mmoja asiyekuwa na mshirika.

Kuchinja hafanyiwi mwengine asiyekuwa Allaah. Mwenye kuchinja kwa ajili ya mwengine asiyekuwa Allaah amefanya shirki. Nadhiri haiwi kwa mwengine asiyekuwa Allaah. Kutimizwa kwake kunakuwa kwa Allah (´Azza wa Jall):

يُوفُونَ بِالنَّذْرِ وَيَخَافُونَ يَوْمًا كَانَ شَرُّهُ مُسْتَطِيرًا

“Wanatimiza nadhiri na wanaikhofu siku ambayo shari yake ni yenye kuenea.” (al-Insaan 76:07)

Vilevile ni lazima kwa mja kutahadhari kutokamana na shirki ndogo kwa aina zake zote. Shirki ya matamshi mtu asiape isipokuwa kwa jina la Allaah:

“Mwenye kuapa kwa asiyekuwa Allaah amefanya shirki.”

Hatumtaji Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) pamoja na mwengine Yeyote kwa utashi. Isipokuwa inatakiwa kuweka neno “kisha”. Kwa mfano Allaah akitaka kisha akataka fulani” na “isingelikuwa Allaah kisha fulani”.  Huu ni mfano tu wa shirki ya matamshi ambayo muislamu anatakiwa kujichunga nayo.

Waja wa Allaah! Miongoni mwa aina kubwa ya shirki ndogo ambayo Mtume wetu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alichelea juu ya Maswahabah zake – ni vipi sisi tusichelei juu ya nafsi zetu – ni kujionyesha. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mtu kuipamba swalah yake kwa sababu anajua watu wanamtazama.”

Mtu akaipamba ´ibaadah yake, kisomo chake na akafanya matendo kwa ajili watu wamsifu. Yote haya ni miongoni mwa khatari kubwa na ni kumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) aina ya shirki ndogo, jambo ambalo limekatazwa na Allaah (´Azza wa Jall).

Hakika Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameeleza kwamba mtu wa kwanza atayetupwa Motoni ni watu aina tatu. Msomi au msomaji, mtoaji swadaqah na mpambanaji. Kuhusu msomaji ataulizwa na Allaah:

“Ni kwa nini ulisoma Qur-aan?” Atasema: “Nimesoma kwa kutafuta uso Wako.” Atamwambia: “Umesema uongo. Ulisoma Qur-aan ili uambiwe kuwa ni msomi. Mpelekeni Motoni.”  Kuhusu mtoaji swadaqah ataulizwa: “Kwa nini ulitoa swadaqah?” Atasema: “Nilitoa swadaqah kwa kutafuta uso Wako.” Atamwambia: “Umesema uongo. Ulitoa swadaqah ili uambiwe kuwa ni mkarimu na mtoaji. Mpelekeni Motoni.”  Kuhusu mpambanaji ataulizwa: “Nimepambana jihaad kwa kutafuta uso Wako.” Atamwambia: “Umesema uongo. Ulipambana jihaad ili kusemwe fulani ni shujaa. Mpelekeni Motoni.”

Kwa hivyo ni lazima kwa mja kuzielekeza ´ibaadah zake zote na wala asimtarajie mwengine isipokuwa Allaah Mmoja hali ya kuwa hana mshirika. Hiki ndio kizuizi cha shirki kubwa na shirki ndogo. Ni lazima kwa mja kujisafisha kwa Tawhiyd. Njia ya yeye kusalimika ni kumpwekesha Allaah hali ya kuwa peke yake hana mshirika.

Mja anatakiwa kuogopa kutumbukia ndani ya shirki kubwa na ndogo. Asijiaminishe nafsi yake. Ibraahiym (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akisema:

وَاجْنُبْنِي وَبَنِيَّ أَن نَّعْبُدَ الْأَصْنَامَ

“Uniepushe mimi na wanangu kuabudu masanamu.” (Ibraahiym 14:35)

ilihali yeye ndiye kiongozi wa Tawhiyd na kiongozi wa wepwekeshaji na ambaye Allaah ameeleza kuwa ni Ummah na mwenye imani safi na kwamba hakuwa miongoni mwa washirikina. Yeye alikuwa akimuomba Allaah (´Azza wa Jall) amuepueshe na ´ibaadah ya kuyaabudu masanamu. Ibraahiym at-Taymiy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Ni nani mwenye kujisalimisha na mtihani baada ya Ibraahiym?”

Kwa hivyo mpwekeshaji na muumini wanapaswa wachelee juu ya nafsi zao kutumbukia ndani ya kumshirikisha Allaah (´Azza wa Jall). Ni mamoja shirki kubwa na ndogo.

Waja wa Allaah! Mkingamo wa pili unaokuwa kwenye njia ya mja anapoelekea kwenda kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) – ukhatari wake ni jambo linalofuata baada ya kumshirikisha Allaah (´Azza wa Jall) – ni mkingamo wa Bid´ah na mambo yaliyozuliwa. Jambo hili ambalo ni kuzusha ndani ya dini amelibatilisha Allaah (´Azza wa Jall) ndani ya Qur-aan na Mtume wetu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amelitahadharisha. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا

“Leo wamekata tamaa wale waliokufuru juu ya dini yenu, hivyo basi msiwaogope na niogopeni Mimi. Leo nimekukamilishieni dini yenu na nimekutimizieni neema Yangu na nimekuridhieni Uislamu uwe dini yenu.” (al-Maaidah 05:03)

Dini imekamilika na haihitajii Bid´ah na mambo yaliyozuliwa. Vilevile haihitajii nyongeza. Hakika yule mwenye kuzidisha ndani yake, akazusha ´ibaadah na akajikurubisha kwa Allaah kwa mambo ambayo hayakufanywa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mtu huyo ni mwenye kudai kwamba dini ni pungufu na kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakukamilisha dini na hakufikisha ubalighisho wa wazi. Bali atakuwa ni mwenye kudai kwamba yeye amekuja na jambo ambalo ni kamilifu zaidi kuliko yale aliyofanya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mwenye kufanya Bid´ah na mambo yaliyozuliwa matendo yake yanakuwa ni yenye kurudishwa usoni mwake na hayakubaliwi. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mwenye kuzua katika amri yetu hii yasiyokuwemo atarudishiwa mwenyewe.”

“Mwenye kufanya matendo yasiyoafikiana na amri yetu atarudishiwa mwenyewe.”

 Mtume wetu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati aliposoma maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´la) juu ya wale wanoafuata maandiko yenye kutatiza. Akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hao ndio wale waliokusudiwa na Allaah. Hivyo tahadharini nao.”

Bi maana wazushi na wale wanaofuata matamanio yao.

Muslim amepokea katika “as-Swahiyh” yake kwamba amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Watakujieni watu wenye kukuelezeni ambayo nyinyi wala baba zenu hawakuyasikia. Ole wenu na Ole wao!”

Tahadharini enyi ndugu juu ya jambo la kuzua katika dini na kufanya ´ibaadah ambazo hazikufanywa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hivi wewe ni mwongofu zaidi kuliko Mtume wa Allaah? Wewe ni mbora kuliko Maswahabah wa Mtume wa Allaah? Je, unateremshiwa Wahy? Je, unajiwa na amri kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) baada ya kukatika kwa Wahy kwa kufa kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)? Kwa hivyo tahadharini kwelikweli kutokamana na mambo yaliyozuliwa na Bid´ah. Kwani ni njia ya maangamivu. Njia ya kusalimika kutokamana na mkingamo huu na kutokamana na jambo hili linalokuzuia kutofika kwa Allaah ni kumfuata Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) peke yake. Kwani mja kwa mambo haya mawili – kujiepusha mbali na shirki na kujiepusha mbali na Bid´ah, kumwabudu Allaah pekee na kumfuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pekee – matendo yake yanakuwa ni yenye kukubaliwa mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala):

فَمَن كَانَ يَرْجُو لِقَاء رَبِّهِ فَلْيَعْمَلْ عَمَلًا صَالِحًا وَلَا يُشْرِكْ بِعِبَادَةِ رَبِّهِ أَحَدًا

“Hivyo yule anayetaraji kukutana na Mola wake basi na atende matendo mema na wala asimshirikishe katika ‘ibaadah za Mola wake yeyote!” (al-Kahf 18:110)

Anatakiwa kufanya matendo mema ikiwa na maana ni mwenye kumfuata Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Asimshirikishe kwa ´ibaadah ya Mola Wake yeyote ikiwa na maana mwenye kumtakasia nia Allaah (´Azza wa Jall) katika mambo yote na ´ibaadah zote. Sharti mbili hizi zikitimia basi matendo yanakuwa ni yenye kukubaliwa mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Ikikosekana moja katika sharti mbili hizi basi matendo yanakuwa na kasoro na hivyo hayakubaliwi mbele ya Allaah (´Azza wa Jall).

Ee Allaah! Hakika sisi tunamuomba utukubalie, tawfiyq na uimara.

Sehemu ya pili

Himdi zote njema anastahiki Allaah. Swalah na salamu zimwendee Mtume wa Allaah, kizazi chake, Maswahabah na wale watakaofuata mwenendo wake.

Amma ba´d:

Waja wa Allaah! Mkingamo wa tatu ambao unamzuia mja katika njia yake ya kwenda kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ni kizuizi cha madhambi na maasi, makubwa na madogo. Hakika mambo hayo yanamzuia mja katika njia yake kwenda kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Njia ya kujikwamua na kuokoka kutokamana nayo ni kutubu na kurejea kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Allaah (´Azza wa Jall) ametutahadharisha kutokamana yale madhambi yenye kuangamiza na madhambi makubwamakubwa:

الَّذِينَ يَجْتَنِبُونَ كَبَائِرَ الْإِثْمِ وَالْفَوَاحِشَ إِلَّا اللَّمَمَ

“Wale wanaojiepusha na madhambi makubwa na machafu isipokuwa makosa madogomadogo.” (an-Najm 53:32)

Allaah (´Azza wa Jall) ametahadharisha ndani ya Kitabu Chake katika Aayah nyingi kufanya madhambi na maasi. Ametahadharisha kutokamana na kuufa, kuiba, uzinzi na mengineyo anayoasiwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala):

وَالَّذِينَ لَا يَدْعُونَ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ وَلَا يَقْتُلُونَ النَّفْسَ الَّتِي حَرَّمَ اللَّـهُ إِلَّا بِالْحَقِّ وَلَا يَزْنُونَ ۚ وَمَن يَفْعَلْ ذَٰلِكَ يَلْقَ أَثَامًا يُضَاعَفْ لَهُ الْعَذَابُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَيَخْلُدْ فِيهِ مُهَانًا

“Wale ambao hawaombi pamoja na Allaah mungu mwengine na wala hawaui nafsi ambayo Allaah ameiharamisha isipokuwa kwa haki na wala hawazini – na atakayefanya hivyo atakutana na adhabu. Ataongezewa adhabu maradufu siku ya Qiyaamah na atadumishwa ndani yake akiwa amedhalilika.” (al-Furqaan 25:68-69)

 Mtume wetu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametahadharisha kutokamana na madhambi makubwa na madogo. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Jiepusheni na madhambi saba yenye kuangamiza.” Wakasema: “Ni yepi, ee Mtume wa Allaah?” Akasema: “Kumshirikisha Allaah, uchawi, uzinzi, kula mali ya mayatima, kula ribaa, kukimbia siku ya vita na kuwatuhumu machafu wanawake wenye kujiheshimu waumini na walioghafilika.”

Haya ni jumla katika madhambi makubwa ambayo Mtume wetu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametutahadharisha nayo. Kwa hiyo tusichukulie wepesi mambo haya. Hakika dhambi zake ni kubwa, janga lake ni khatari na khatari yake ni kubwa kwa mja katika dunia na Aakhirah yake. Anatakiwa kujitahidi katika kumwabudu Mola Wake, kurejea kwa Mola Wake na kurudi kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Vilevile anatakiwa kujiepusha na madhambi madogo na asichukulie wepesi kwayo. Mtu hatakiwi kufikiria kuwa ni madhambi madogo ambapo baadaye akayachukulia wepesi. Kukusanyika kwa madhambi madogo ndani ya moyo ni kitu kinachomwangamiza mja, kama alivosema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Tahadharini na yale madhambi yenye kudharauliwa. Tahadharini na yale madhambi yenye kudharauliwa. Mfano wa madhambi haya yenye kudharauliwa ni kama mfano wa watu walioshuka kutoka kwenye mlima. Kila mmoja katika wao amekuja na fimbo mpaka wakakonga moto mkubwa.”

Namna hii ndivo yanakuwa madhambi makubwa yanapokusanyika moyoni kwa mtu. Mtu anafanya dhambi dogo, kisha anafanya dhambi nyengine dogo na hatimaye anachukulia wepesi madhambi madogo mpaka yanakusanyika ndani ya moyo wake. Tahamaki yanamwangamiza.

Ee mja wa Allaah! Usitazame udogo wa dhambi. Bali tazama ukubwa wa Yule unayemuasi. Usitazame udogo wa dhambi unayofanya badala yake tazama ukubwa wa Yule unayemuasi.

Hapana shaka kwamba mja katika njia yake ya kwenda kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) juu ya mikingamo hii inayomkabili anapaswa kutambua kuwa kurejea kwake kwa Allaah (´Azza wa Jall) Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amewafunguilia mlango waja Wake pale wanapotaka. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) baada ya kutaja madhambi haya – shirki, kuua na uzinzi – akasema:

إِلَّا مَن تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ عَمَلًا صَالِحًا فَأُولَـٰئِكَ يُبَدِّلُ اللَّـهُ سَيِّئَاتِهِمْ حَسَنَاتٍ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا وَمَن تَابَ وَعَمِلَ صَالِحًا فَإِنَّهُ يَتُوبُ إِلَى اللَّـهِ مَتَابًا

“Isipokuwa yule aliyetubu na akaamini na akatenda matendo mema, basi hao Allaah atawabadilishia maovu yao kuwa mema na Allaah daima ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu. Na atakayetubu na akatenda mema, basi hakika yeye anatubia kwa Allaah tawbah ya kweli.” (al-Furqaan 25:70-71)

Hii ndio rehema ya Mwingi wa rehema. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ambaye ni mkwasi kwetu, kutokamana na matendo yetu na utiifu wetu. Mola Wetu (Subhaanahu wa Ta´ala) ni mkwasi kutokamana na waja Wake. Yeye hanufaiki kwa mema yetu na wala hadhuriki kwa maasi yetu:

“Anakunjua mikono Yake usiku atubie ambaye alikosea mchana na anakunjua mikono Yake mchana atubie ambaye alikosea usiku mpaka pale jua litapochomoza kutoka upande wake wa magharibi.”

Mola Wetu ambaye ni mkwasi na viumbe Wake hushuka mwishoni mwa kila usiku katika theluthi ya mwisho ya usiku na akawanadi waja Wake:

“Ni nani mwenye kuniomba nimuitikie? Ni nani mwenye kuniomba nimpe? Ni nani mwenye kuniomba msamaha nimsamehe?”

Kwa hivyo mlango wa tawbah uko wazi. Lakini mja anahitaji wakati wa kutubia na kurejea kwake kwa Allaah kuitakasa nia yake kwa Allaah (´Azza wa Jall) katika tawbah yake. Vilevile anatakiwa kufanya maazimio yenye nguvu kutorudi katika dhambi. Hakika Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Achukie kurudi kwenye ukafiri kama anavyochukia kutupwa kwenye moto.”

Vivyo hivyo anatakiwa kujutia yale aliyoyafanya na ajutie yale aliyokusuru katika upande wa Allaah. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Tawbah ni kule kujutia.”

Kadhalika anatakiwa kujivua kutoka katika dhambi na kutoiendeleza:

وَلَمْ يُصِرُّوا عَلَىٰ مَا فَعَلُوا وَهُمْ يَعْلَمُونَ

“… na hawaendelei katika waliyoyafanya na wao wanajua.” (Aal ´Imraan 03:135)

Anatakiwa pia kurudisha haki za watu kwa wenye nazo ikiwa dhambi hiyo inahusiana na haki za waja.

Akihakikisha sharti hizi, akakithirisha kumuomba Allaah msamaha, akamwelekea Mola Wake na akatubia na kurejea Kwake kwa moyo msafi, wenye huruma na wenye kujutia, basi Allaah atamsamehe. Bali fadhilah za Allaah ni zenye wasaa zaidi. Allaah atayageuza maovu yake yawe mema, amsamehe, ampandishe daraja za juu na amfungulie milango ya kheri.

Swalah na salamu zimwendee Mtume wetu Muhammad.

  • Mhusika: Shaykh Khaalid bin Dhwahwiy adh-Dhwafayriy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Masjid al-Irshaad Ilala Dar es Salaam 1441 Rabiy´ ath-Thaaniy 09
  • Imechapishwa: 07/12/2019